Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa miezi mitatu kwa Mkandarasi anayejenga barabara ya Mnivata – Mitesa (km 100), kuhakikisha wanakamilisha kilometa 50 za barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kuufungua Mkoa wa Mtwara kiuchumi na kuunganisha Wilaya mbalimbali za mkoa huo.
Ulega ametoa agizo hilo katika ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Mtwara ambapo pamoja na mambo mengine amekagua maendeleo ya barabara ya Mnivata – Newala – Masasi na kuzungumza na wananchi katika vijiji mbalimbali vinavyopitiwa na mradi huo na kusisitiza kukamilika kwa barabara hiyo kwa viwango vya ubora.
Ameongeza kuwa ni maelekezo ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miradi mipya ya ujenzi wa barabara iende sambamba na uwekaji wa taa za barabarani katika miji au vijiji.
Waziri Ulega ameeleza kupitia miradi hiyo ya barabara katika Mkoa wa Mtwara na Lindi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa ajili ya utekelezaji wake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya barabara, huduma za kijamii, biashara na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya barabara na kuwataka wananchi kulinda miundombinu hiyo ili idumu na kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdallah Chikota, amesisitiza umuhimu wa wananchi wanaoishi jirani na mradi kupewa kipaumbele katika ajira zisizo za kitaalamu. Pia amepongeza mpango wa kufungwa kwa taa za barabarani, akieleza kuwa utasaidia kuongeza usalama na kukuza shughuli za biashara nyakati za usiku.
Awali, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Emil Zengo, amesema mradi huo unatekelezwa na wakandarasi wawili, Sehemu ya kwanza kutoka Mnivata hadi Mitesa (km 100) inayojengwa na China Wu Yi imefikia asilimia 56.4 ya utekelezaji, huku sehemu ya pili ya kutoka Mitesa hadi Masasi (km 60) inayotekelezwa na China Communications Construction ikifikia asilimia 75.4