Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba amesema Serikali itaijenga kwa kiwango cha lami mradi wa barabara ya Musoma Vijijini-Makojo-Busekela km 92 ili kuchochea uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.

Akizungumza na wananchi wa Musoma Vijijini mkoani Mara, Dkt.Nchemba amesema ujenzi huo ni utekelezaji wa ahadi za Serikali kwa wananchi ili kuboresha miundombinu na kuhamasisha maendeleo.

“Wizara ya Ujenzi hakikisheni taratibu za kusaini mkataba na mkandarasi wa kujenga barabara hii zinakamilika haraka ili ujenzi uanze mara moja kwa km 40 za kwanza”, amesisitiza Waziri Mkuu Dkt. Nchemba.

Naibu Waziri wa Ujenzi Eng.Godfrey Kasekenya amesema barabara hiyo inajengwa kwa awamu ambapo tayari km 5 zimekamilika sehemu ya makao makuu ya Halmashauri ya Musoma vijijini.

Eng.Kasekenya ameeleza kuwa Mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo na taratibu za kusaini mkataba zinaendelea ambapo zimefikia katika hatua nzuri ifikapo mwezi Agosti ujenzi wa mradi huo utaanza kwa sehemu ya kilomita 40.

Naye Mbunge wa Musoma Vijijini Prof.Sospeter Muhongo amepongeza na kuomba Serikali kuendelea na ujenzi wa barabara ya Musoma Mjini-Suguti-Makojo hadi Busekela kwa ajili ya kurahisisha shughuli za kilimo,uvuvi usafiri na usafishaji kwa wananchi wa eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *