Baadhi ya Madereva wa Bajaji maeneo ya Tegeta Kibaoni, jijini Dar es Salaam, wamelalamikia hospitali binafsi ya Kitengule kufanya uchafuzi wa mazingira unaohatarisha afya zao.

Madereva hao wamesema hospitali hiyo inatiririsha maji taka kwenye mifereji ya maji ya mvua barabarani na kuchoma taka za hospitali kusababisha moshi kutapakaa maeneo hayo na kuathiri afya zao.

Akizungumza na Morningstar post, Bw Fred Deogratus ambaye ni afisa habari wa umoja wa madereva wa Bajaji Kibaoni, alisema kero kubwa katika maeneo hayo ni mbili.

Alisema hospitali ya Kitengule imepitisha bomba za maji taka na kuyaelekeza kwenye mitaro ya maji ya mvua, hivyo imekuwa ni kero kubwa kwa wakazi na abiria wanaokuja kupanda usafiri wa bajaji.

“Kero nyingine inayotusumbua hapa ikifika saa tano usiku wanachoma taka za hospitali na moshi unasambaa maeneo yote hivyo, kusababishia kero sana, tunaomba watu wa mazingira waliangalie hili kwa kuwa limekuwa kero kubwa kwetu,” alisema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Wazo Bw. Medard Mashauri, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo hakuweza kupatikana mara moja ila juhudi za kumpata zinaendelea.

Mjumbe wa shina mtaa wa wazo Bakar Mbegu alikiri kuwepo kwa moshi unaotapakaa maeneo yote ya makazi ya watu na kusababisha usumbufu mkubwa.

Hata hivyo uongozi wa hospitali ya Kitengule ulipotafutwa kuzungumzia suala hili haukuweza kupatikana mara moja. Morningstar post inaendelea kuwatafuta na mamlaka zinazohusika kutoa ufafanuzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *