NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya JINLING Investment ya jijini Dar es Salaam, inayomilikiwa na raia kutoka China, inadaiwa kufanya shughuli zake bila kuzingatia taratibu za usalama kwa wafanyakazi wake.

Taarifa za uhakika kutoka kwenye vyanzo vyetu vilivyopo ndani ya kampuni hiyo vinadai, wafanyakazi wa kampuni hiyo inayojihusisha na uchanganyaji wa zege, wanafanya kazi kwenye mazingira magumu na kuhatarisha maisha yao.

Chanzo hicho kilisema, wafanyakazi wengi hawana mikataba ya ajira, hawana bima na vitendea kazi vinavyoendana na shughuli wanazofanya na kusababisha madhara.

“Hivi karibuni kumetokea tukio moja ambalo limesababisha hofu kubwa kwa sisi wafanyakazi, yupo mwenzetu mmoja amefariki baada ya kupigwa na shoti ya umeme akiwa ndani ya gari,” kilisema chanzo hicho.

Kilisema, uzembe uliosababishwa na dereva wa gari namba T 264 EPF linalomilikiwa na kampuni hiyo, ndio chanzo cha kugusa waya na kupiga shoti gari hilo na kusababisha kifo cha kijana anayeitwa Hatibu Shabani, aliyekuwa Mwendesha Mashine Msaidizi wa kampuni hiyo.

“Lile gari wakati likimwaga zege ‘site’ likagusa waya wa umeme na kusababisha shoti iliyolipiga gari hilo na kumuumiza marehemu mguuni na kichwani na kusababisha kifo chake,” kilisema chanzo chetu.

Aidha, mwandishi wa habari hii alifanya jitihada za kuchunguza zaidi tukio hilo ili kubaini hatua zaidi zilizochukuliwa, ambapo ilibainika kulifunguliwa faili namba OBEY/RB/6134 kwenye kituo cha polisi Osterbay.

Uchunguzi umebaini kuwa hakuna mtu yeyote aliyeshikiliwa kuhusika na tukio hilo, huku ikidaiwa hakuna uchunguzi wowote uliofanyika kubaini mazingira halisi ya kifo cha kijana huyo anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 27 hadi 35.

Alipotafutwa Injinia Laurent Chungu, Msimamizi wa mradi huo uliopo maeneo ya Mwananyamala Bwawani, alikiri kutokea kwa tukio na kuwekwa wazi kwamba, linahusisha kampuni ya JINGLIN na sio kampuni yao.

Hata hivyo, uchunguzi zaidi wa Morning StarPost imebaini kuwa, mradi huo una mapungufu mengi ya kiusalama, ambapo hakuna kingo za kuzuia vitu visiangukie kwenye nyumba za jirani ikiwemo misumari na nondo.

Kwa upande wake, Afisa Rasilimali Watu wa kampuni ya JINLIN aliyejulikana kwa jina moja la Vicky naye alikiri kutokea kwa tukio hilo ambalo lilitokea Septemba 1, 2026, majira ya jioni, ingawa hakuwa tayari kuzungumza zaidi.

Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Mtatiro Kitinkwi hazikuzaa matunda, ambapo simu yake ya mkononi iliita bila majibu muda wote alipotafutwa.

Waandishi wa Morning StarPost wanaendelea kufuatilia kwa kina tukio hilo na ripoti zaidi itatolewa ili Mamlaka husika zichukue hatua na kudhibiti vitendo vya waajiri hususani wa kampuni zinazomilikiwa na raia wa China kutozingatia taratibu za ajira na usalama wa wafanyakazi wawapo kwenye majukumu yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *