
Jengo la kiwanda cha kuzalisha na kutengeneza chakula cha mifugo cha Backbone

Mfereji wa maji taka unatoka kwenye kiwanda cha Backbone ukilekezwa kwenye mifereji ya maji ya mvua mbarabarani
Kiwanda cha kuzalisha chakula cha mifugo, Backbone, kilichopo Kata ya Misugusugu Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani, kinadaiwa kukiuka sheria za nchini.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Morningstar Post, kiwanda hicho kimefunga matenki ya dizel yenye pampu ya mafuta, bila ya kufuata sheria na kanuni za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
EWURA haijaruhusu kila mtu au kila kiwanda kufunga tu matanki ya dizeli yenye pampu (Consumer Installation) kiholela, ili ustawi na usalama wa miundombinu hiyo unadhibitiwa vikali kisheria.
Ili kiwanda binafsi kiruhusiwe kufunga tanki kubwa la dizeli na pampu yake kwa ajili ya matumizi ya mitambo au magari yake, lazima kipate kibali cha ujenzi na leseni ya uendeshaji kutoka EWURA.
Kitaalamu, miundombinu hii inaitwa Consumer Installation Facility (Kituo cha Mafuta cha Matumizi Binafsi), na imeweka masharti Kiwanda au mmiliki hawezi kununua tu tanki na pampu na kuanza kuvitumia. Ni lazima akidhi vigezo hivi kupitia mfumo wa EWURA unaoitwa LOIS (Licensing and Order Information System):
Kibali cha Ujenzi (Construction Approval): Kabla ya kufunga tanki na pampu, ni lazima EWURA wakague ramani na eneo ili kuhakikisha kuna usalama wa kutosha dhidi ya majanga ya moto na mazingira.
Leseni ya Uendeshaji (Consumer Installation License): Baada ya ujenzi kukamilika, EWURA hutoa leseni ya uendeshaji kulingana na ukubwa wa kiwanda.
Serikali ilipiga marufuku kwa watu kufunga pampu za mafuta isipokuwa kwa watu maalumu walio tajwa kwenye sheria hiyo mfano migodini, mashamba makubwa ambayo yana mitambo isiyo tembea nk. Pia ewura wathibitishe sifa hizo kwa kushirikiana na mamlaka zingine za serikali zikiwemo halmashauri za miji husika.
Uchunguzi wa tovuti hii ya habari za uchunguzi umebaini kuwa kiwanda hicho hutiririsha maji machafu yanayotoka kwenye kiwanda hicho na kuyaelekeza kwenye mitaro ya maji ya mvua ya barabara ya morogoro na kusababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira.
Juhudi za Morningstar post kumpata mkurugenzi wa manispaa hiyo ili kuzungumzia tuhuma hizi hazikuweza kufanikiwa mara kadhaa waandishi wetu waliambiwa yuko kwenye ziara za viongozi wa kitaifa wanaotembelea manispaa hiyo kwa upande wa serikali za mitaa.
Afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa sio msemaji wa manispaa alikiri kuwepo kwa tuhuma hizo.
Akijubu tuhuma hizo msemaji wa kiwanda hicho aliyejitambulisha kwa jina moja la Ali, alikiri kutiririsha maji machafu ya kiwanda kwenye mifereji ya maji ya mvua na kufunga matenki hayo ya mafuta akidai EWURA wametoa kibali.
Backbone ni kiwanda kinachomilikiwa na wafanyabiashara raia wa kutoka China kinazalisha na kutengeneza chakula cha mifugo ikiwemo vifaranga vya kuku. Morningstar post inaendelea kutafuta taarifa zaidi kwa mamlaka husika.