OWM-TAMISEMI, Iringa

Serikali imesema itaendelea kuendeleza waamuzi vijana ili kuwezesha Taifa kuwa na idadi kubwa ya wataalamu wa michezo nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Profesa Riziki Shemdoe, wakati akifunga rasmi mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Mkoani Iringa.

Profesa Shemdoe amesema katika mashindano ya mwaka huu kulikuwa na waamuzi vijana 22 ambao walishiriki kusimamia sheria na kanuni za michezo hiyo.

“Hii ni hatua kubwa ambayo Serikali tumepanga kuendeleza ili kupata wataalamu wengi zaidi watakaoajiriwa katika sekta hiyo ndani na nje ya nchi”amesema Profesa Shemdoe.

Ameelezea pia juu ya kuendelea kuboresha miundombinu ya michezo na Sanaa, kwa kuhakikisha kuwa shule zote nchini zinakuwa na viwanja vya kuchezea.

Amekumbushia pia kuzingatia uendelezwaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kwa kuwawekea mazingira rafiki ya kuchezea sambamba na waalimu wenye sifa.

UMITASHUMTA & UMISSETA 2026 iliandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), ikishirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo.

Kauli mbiu ya UMITASHUMTA & UMISSETA 2026 ni “Michezo na Sanaa Shuleni: Daraja la Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *