Na OWM – TAMISEMI, Iringa
Mkurugenzi wa Kitengo cha Michezo, Utamaduni na Sanaa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Ndg. Yusuph Singo, amewataka Maafisa Michezo na Utamaduni wa mikoa na halmashauri nchini kuendelea kudumisha umoja, ushirikiano na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Singo ametoa wito huo Juni 24, 2026, wakati akifungua mafunzo ya upimaji wa utendaji kazi kwa Maafisa Michezo na Utamaduni wa mikoa na wilaya yaliyofanyika mkoani Iringa.
Akizungumza katika mafunzo hayo, amesema mafanikio ya taasisi yoyote yanategemea kwa kiasi kikubwa mshikamano wa watumishi wake, ushirikiano katika utendaji wa kazi na uwajibikaji wa kila mmoja katika nafasi aliyonayo.
Ameeleza kuwa katika kipindi hiki ambacho sekta mbalimbali zinaendelea kupitia mabadiliko ya kiutendaji, watumishi wanapaswa kuwa tayari kufanya kazi kwa pamoja, kubadilishana uzoefu na kusaidiana ili kufikia malengo ya taasisi kwa ufanisi zaidi.
“Majukumu yenu ni muhimu sana katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki. Hivyo ni lazima tufanye kazi kwa umoja na ushirikiano, tukitambua kwamba mafanikio ya mmoja ni mafanikio ya taasisi nzima,” amesema Singo.
Aidha, amesisitiza kuwa mabadiliko ni sehemu ya maendeleo ya kiutendaji, hivyo ni muhimu kwa watumishi kuyapokea kwa mtazamo chanya na kushirikiana katika utekelezaji wake ili kuongeza tija, ufanisi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Singo amesema kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia kuimarisha mahusiano mema mahali pa kazi, kuongeza uwajibikaji na kuleta matokeo chanya yatakayochangia maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla