Mfanyakazi anayefanya kazi kwenye mradi mkubwa wa  ujenzi  wa Soko la Kimataifa la Biashara la Afrika Mashariki (EACLC), Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye alijeruhiwa akiwa kazini bila kulipwa fidia.

Na MWANDISHI WETU

WAFANYAKAZI wa Kampuni za ujenzi za Wachina zinazojenga soko la Kimataifa la Biashara la Afrika Mashariki (EACLC), Ubungo jijini Dar es Salaam, ilipokuwa standi ya mabasi ya mkoa, inadaiwa wananyanyaswa na wachina.

Pia, taarifa zaidi Morningstar Post imezipata zinadai, baadhi ya kampuni za ujenzi kwenye mradi huo mkubwa, hazifuati kanuni za ujenzi na miongozo mbalimbali iliyowekwa na mamlaka za serikali.

Taratibu za ujenzi zinazosimamiwa na Bodi ya Wakandarasi Nchini (CRB), Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), baadhi hazitekelezwi kwenye mradi huo.

Wakizungumza na Morningstar Post wafanyakazi ambao hawakupenda majina kuwekwa wazi wakihofia kupoteza kibarua chao, walidai kuwa licha ya kufanya mradi mkubwa kama huo, lakini hawapewi vitendea kazi vinavyo stahili wakati wa kazi.

“tunapokuwa kwenye ujenzi hatupewi vitendea kazi, hivyo kusababisha kupata majeraha ya mara kwa mara na wakati mwingine imesababishia vifo kwa wenzetu na ulema wa kudumu bila kupata fidia zozote kwa kuwa hawajaadikishwa mfuko wa fidia ya wafanyakazi (WCF), licha ya serikali kusisitiza mara kwa mara kampuni kuwaandikisha wafanyakazi wao,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

Morningstar Post ilitembelea eneo la mradi huo Ubungo kwa lengo la kupata ufafanuzi wa tuhuma za unyanyasaji kwa wafanyakazi unaofanywa na Wachina.

Hata hivyo, Mchina mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Andy ofisini kwake kwenye jengo la Ubungo Plazza, hakutaka kuzungumza zaidi suala hilo na kusisitiza kampuni yao haihusiki.

Aliongeza kuwa kampuni yao imewapa zabuni kampuni ya CCECC ndio wanaojua kampuni zinazojenga mradi huo ambazo zote ziko chini yao.

Alipoulizwa kuwa idadi ya watu wangapi wamepoteza maisha kwenye mradi huo, kwa kufanya kazi kwa kukosa vitendea kazi alikanusha kuwa hajui jambo lolote.

Morningstar Post inaendelea kufuatilia taarifa ijayo itachapisha orodha ya majina ya watu wote walioathirika na mradi huo bila malipo yoyote ya fidia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *