Mhe. Mbunge wa Nanyumbu Yahaya Mhata
Na Mwandishi Wetu
WANANCHI wa Wilaya ya Nanyumbu Mkoa wa Mtwara, wamemlalamikia mbunge wao kushindwa kufuatitilia na kutatua matatizo yao.
Wamesema mbunge wao tangu amechaguliwa amekuwa hatembelei jimboni katika baadhi ya vijiji kujua shida na changamoto mbalimbali za wananchi.
Wakiongea na mwandishi wa Morningstar Post kwa njia ya simu baadhi ya wananchi hao walidai kwamba mbunge wao Yahaya Mhata anathamini watu wenye fedha.
Wanadai kuwa amekuwa anathamini na kutembelea watu wenye uwezo wa fedha maeneo ya mjini peke yake, na kutengeneza matabaka miongoni mwao wilayani humo.
Walisema awali alivyopata ubunge alikuwa angalau anatembelea kwenye jimbo lakini baada ya kuchaguliwa aliwasahau wapiga kura wake na kuona hawana maana tena.
“Wakati wa karibu na uchaguzi anakuja kutwa mara tatu jimboni,” walisema kwa hasira.
Wakaongeza kuwa mbunge huyo hivi sasa anafanya kampeni za chini kwa chini kuwaweka viongozi wa mtaa ili baadae wamsaidie kwenye uchaguzi ujao.
Kwa upande wake akizungumzia madai hayo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nanyumbu Bw. Rashidi Mrope alisema hana taarifa za malalamiko hayo.
“Labda wanafanya kampeni kwa siri…nitaanza kufuatilia jambo hilo.” alisema Mrope.
Morningstar Post, alipomtafuta mbunge wa jimbo hilo Mh. Mhata hakuweza kupatikana kwenye simu yake ilikuwa inaita bila majibu.
Hata hivyo, tunaendelea kumtafuta Mhe. Mhata kuzungumzia taarifa hizo za wapiga kura wake.