BAADA ya kupokea kipigo cha aibu, Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameibuka kwa kusema kipigo hicho kimeacha maumivu ya kudumu kwa kila Mwanasimba, hivyo wanatakiwa kusahau kilichotokea na kuganga yajayo.
Simba ilipoteza mchezo wake wa kwanza msimu huu 2023/24 dhidi ya Yanga kwa kukubali kichapo cha mabao 5-1, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Sasa, Ahmed Ally ameibuka baada ya kukiri aliondoka uwanjani mapema kwa kisingizio cha kuhofia mvua, zinazoendelea kunyesha jijini Dar, baada ya kutafutwa na waandishi wa bila mafanmikio.
Hivyo basi, leo mchana ameibukia katika mitandao yake ya kijamii akiwalenga mashabiki na wanachama wa Simba ambao bado hali zao sio njema, kutokana na kilichonekana jana Jumapili (Novemba 05).
Katika kurasa zake za kijamii Ahmed Ally amendika; “Kwenye mkutano wa wanahabari nilisema, hii ni mechi ambayo matokeo yake huwa yanaacha furaha ya kudumu au huacha maumivu ya kudumu kwenye mioyo ya mashabiki wake, bahati mbaya ni sisi ndo tunabaki na maumivu ya kudumu.
Kila Mwanasimba anawaza sababu tafauti tofauti iliyosababisha tupoteze mchezo wa jana (Jumapili ya Novemba 5, 2023) iko namna sahihi ya kujua sababu hizo nayo ni utulivu tuwape viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wetu utulivu wa kujitathmini kwa maslahi ya mechi zijazo,” aliandika kuongeza.
“Novemba 9 kuna mchezo dhidi ya Namungo hivyo ni vema tukajikita zaidi kuangalia tunachukuaje alama tatu hizo baada ya kupoteza za jana Let’s go Wana Lunyasi sifa ya timu kubwa ni kuweza kuhimili nyakati ngumu kama hizi,” alimaiza kuandikka.