NA Kalume Kazungu
HUKU ulimwengu leo Jumatano ukiadhimisha Siku ya Kukumbukwa kwa Biashara ya Utumwa na Marufuku yake, viongozi wa dini, wazee na watetezi wa haki za binadamu, Kaunti ya Lamu, Mombasa wamepongeza kusitishwa kwa biashara hiyo waliyoitaja kuwa ya kikoloni na dhalimu.
Siku ya Kimataifa ya kukumbuka biashara ya utumwa na kupigwa kwake marufuku huadhimishwa tarehe 23 Agosti ya kila mwaka.
Wakizungumza kisiwani Lamu, viongozi wa dini ya Kiislamu hata hivyo walikinzana na hatua ya kutengwa kwa siku maalum ya kukumbuka biashara ya utumwa duniani, wakishikilia kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuurejesha ulimwengu katika enzi za giza.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (SUPKEM) tawi la Lamu, Mohamed Abdulkadir, masheikh na maimamu hao walichacha kwamba enzi za utumwa ni za kuvunja moyo na kwamba hawaoni sababu masuala kama hayo yaliyokuwa yenye kudhalilisha binadamu yakumbukwe katika ulimwengu wa leo wa karne ya 21.
Bw Abdulkadir alisema katu haoni la kujivunia na linalofaa kukumbukwa katika biashara ya utumwa kwani mbali na kukiuka haki za binadamu, biashara hiyo ni kinyume cha dini ya kiislamu.
Kulingana na Bw Abdulkadir, Uislamu ulikataza kununua watumwa na kuwamiliki.
Alifafanua kwamba miaka kabla ya kuja kwa Uislamu, utumwa uliendeshwa kiholela.
Watu waliokuwa wanadaiwa walifanywa watumwa, mateka wa kivita, ama hata kuuawa.
Kwenye mataifa yaliyokuwa dhaifu, watu waliwindwa kama wanyama, wakauawa au kutekwa na kufanywa watumwa.
Bw Abdulkadir alisema Uislamu katika hali isiyo ya utatanishi, uliwakataza wafuasi wake kuwafanya binadamu wenzao watumwa kwa kisingizio chochote kile.
“Leo ulimwengu ukiadhimisha kumbukumbu ya biashara ya utumwa na kupigwa kwake marufuku, sisi kama viongozi wa dini tunaunga mkono kusitishwa kwa biashara hiyo mbovu. Hata hivyo tunapinga maadhimisho ya siku kama ya lao eti dunia kukumbuka enzi za biashara ya ukoloni na utumwa. Kufanya hivyo ni sawa na kuurejesha ulimwengu katika karne ya giza na madhila. Vile biashara hiyo ilitokomezwa ilifaa isahaulike kabisa katika fikra za waja,” akasema Bw Abdulkadir.
Kabla ya Uislamu, watu wenye nguvu, na wapendao kutawala wengine kuwa watumwa, walikuwa na desturi ya kuwafanya watumwa binadamu wenzao walio dhaifu bila kusita.
Muhimu miongoni mwa sababu nyingi za kuwafanya watu wengine watumwa ni vita, ambapo mshindi aliweza kufanya chochote anachotaka kwa adui aliyemshinda.
Angeweza kuwauwa wapiganaji waliokamatwa mateka, angewafanya kuwa watumwa au pengine kuwaweka chini ya mamlaka yake au makucha yake.
“Pia utawala, hasa mkuu wa mtawala angeweza kumtia utumwani, kutegemeana na hiari yake ipendavyo, mtu yeyote aishiye katika himaya yake. Utapata kwamba Uislamu ulipotokeza, ulibatilisha na kutangulia sababu mbili za mwisho kabisa. Hakuna mtawala au mlezi aliye ruhusiwa kuwafanya raia wake au watoto wake kuwa watumwa wake. Kila mtu alipewa haki zake kikamilifu; mtawala na mtawaliwa, mzazi na mtoto walitakiwa kuishi katika mipaka iliyowekwa na dini. Hakuna mtu aliyeruhusiwa kukaidi mipaka hiyo,” akasema Bw Abdulkadir.
Ustadh Omar Shee alisema kupigwa marufuku kwa biashara iliyokuwa ikiendelea ulimwenguni ya utumwa kulishabihiana na mafundisho ya Allah katika Kurani yanayoweka wazi waumini kwamba ukitaka kwenda peponi basi lazima umwachie mtumwa huru.
“Aya katika Kurani inatupa wosia kwamba njia ya kutufikisha peponi ni kumpa mtumwa ungwana. Twapongeza kabisa hatua iliyochukuliwa kuangamiza biashara ya utumwa ulimwenguni. Hilo la kukomesha hiyo biashara ndilo lililokuwa muhimu ila sioni maana ya waja leo hii kujipa kumbukumbu ya biashara ya ukoloni na utumwa. Huko ni sawa na kututonesha makovu ya utumwa ambayo yafaa tuyafute kabisa kwenye fikra zetu,” akasema Bw Shee.
Kwa upande wake, Mshirikishi wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Muslims for Human Rights (MUHURI), kaunti ya Lamu, Mohamed Skanda alitaja watumwa kuwa bidhaa ya biashara kwa wakati huo, hali ambayo ilikuwa sawa na kukaidi haki za binadamu.
Mshirikishi wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la MUHURI, Mohamed Skanda akihutubia wanahabari. Anasifu kupigwa marufuku kwa biashara ya utumwa akiitaja kuwa ukiukaji wa haki za kimsingi za binadamu.
Kulingana na Bw Skanda, utumwa ulikuwa chanzo cha kupatia maisha kwa maelfu ya watu na chanzo cha kazi kwa maelfu ya wengi.
“Jinsi mtu alivyokuwa na idadi kubwa ya watumwa katika himaya yake basi tayari ilimaanisha kuwa alama ya hadhi kwake, ambacho ni kinyume kabisa cha haki za binadamu. Tunapoadhimishja siku ya kukumbuka biashara ya utumwa na jinsi ilivyopigwa marufuku ulimwenguni, ni vyema tuzidishe nguvu katika kuutokomeza utumwa Kenya, Afrika na duniani kwa ujumla., Utumwa ni ukaidi wa haki za binadamu,” akasema Bw Skanda.
Kwingineko, wazee wa Lamu wanasema licha ya biashara ya utumwa kupigwa marufuku, baadhi ya mataifa ya Afrika na ulimwengu bado yanaendeleza utumwa dhidi ya mataifa madogomadogo.
“Sisi twahisi utumwa bado upo hadi leo. Kwa mfano, Afrika tuko na maadili yetu ya kimsingi lakini utapata baadhi ya mataifa yenye nguvu kama vile Amerika hupenda sana kutuzuia kufanya maamuzi kivyetu. Itakuwaje nchi kama vile Uganda kupiga marufuku ushoga na usagaji na kisha nchi zenye ushawishi mkubwa zikiiwekea nchi hiyo vikwazo? Utumwa utakoma kabisa ulimwenguni ikiwa mataifa yenye ushawishi yataacha kukandamiza mataifa madogomadogo na yanayotegemea misaada kutoka ulaya,” akasema Bw Hamadi Mahmoud, mzee wa Lamu.
Wazee hao pia walitaja ufisadi ulioenea Kenya na mataifa mengine mengi, ubaguzi wa rangi, utovu wa usalama na maovu mengine kuwa miongoni mwa mambo wanayoyachukulia kuwa utumwa-mamboleo.
Ukomeshaji wa biashara ya watumwa ni mchakato au mlolongo wa matukio yaliyopelekea ufutaji au usitishaji wa biashara hiyo katika karne ya 19.
Kwa jumla, biashara ya watumwa ulimwenguni ilikuwa ni yenye kudhalilisha utu wa binadamu, hasa Waafrika ambao ndio waliotumika kwa kiasi kikubwa katika biashara hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *