Na Mwandishi Wetu
Ujenzi mkubwa wa jengo la ghorofa moja linajengwa maeneo ya Kifuru, Ilala jijini Dar es Salaam bila ya vibali vya ujenzi.
Morningstar Post ilifika kwenye jengo hilo linalojengwa maeneo ya Kifuru maeneo ya Hali ya Hewa na kushuhudia ujenzi mkubwa unajengwa na mafundi wa mtaani.
Wakizungumza na Morningstar Post, Fundi Mkuu aliyekutwa eneo la ujenzi ambaye alijitabulisha kwa jina la Dimoso alikiri kuwa mradi huo haujasajiliwa na hakuna kampuni inayohusika kufanya ujenzi hapo licha ya kuwa ni mradi wa mamilioni ya shilingi.
“Mimi ndio fundi mkuu na ndio injinia lakini mambo mengine yote aulizwe mwenye jengo, alisema Dimoso.
Akizungumza na Morningstar Post, msimamizi wa jengo hilo ambaye hakujitambulisha jina baada ya kuwasiliana na mmiliki wa jengo hilo Bw. Yassin Bakari alijibu kuwa waandishi wa habari wafike na barua kutoka kwa mtendaji ili kupata haki ya kuhoji uhalili wa ujenzi unaofanyika bila vibali
Hata hivyo Morningstar POST inaendelea kumtafuta mhandisi wa jiji na viongozi wa Bodi ya Wakandarasi kuzungumzia suala hilo la ujenzi mkubwa kufanyika bila vibali na hivyo kuikosesha serikali mapato na kukiuka taaratibu za nchi.
