
Mkuranga, Pwani —
Malighafi zenye uzito wa tani 200 zilizokuwa zikihifadhiwa nje ya kiwanda cha Hoota Co. Ltd, kilichopo eneo la Vikindu, Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, zimeteketea kwa moto.
Kwa mujibu wa ripoti ya kikosi cha zima moto na uokoaji nchini, moto huo unadaiwa kuwa ulisababishwa na uzembe wa mafundi waliokuwa wakichoma moto kwa lengo la kusafisha eneo kwa ajili ya ujenzi wa mtaro.
Tukio hilo limetokea Oktoba 11, 2026, ambapo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kupitia Kituo cha Mkuranga lilipokea taarifa ya tukio hilo walifanikiwa kuzima moto huo uliokuwa ukiendelea kuwaka kwenye malighafi zilizokuwa zimehifadhiwa nje ya kiwanda hicho, ambacho awali kilikuwa kikitengeneza viatu vya aina ya yeboyebo na sasa kinajulikana kwa utengenezaji wa klipsi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, kikosi kilifanikiwa kuudhibiti na kuuzima moto huo baada ya kufanya kazi ya uokoaji na uzimaji kwa muda wa takribani saa nne na nusu.
Pamoja na uharibifu wa malighafi hizo, hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa wala kupoteza maisha katika tukio hilo. Aidha, majengo yote ya kiwanda hicho yaliokolewa na moto, hivyo kuzuia madhara makubwa zaidi ambayo yangetokea iwapo moto huo ungeenea hadi kwenye majengo.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetoa wito kwa wamiliki wa viwanda na wafanyabiashara kuhakikisha malighafi zinahifadhiwa kwa kuzingatia kanuni za kitaalamu za usalama wa moto, pamoja na kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa zimamoto ili kuepusha majanga yanayoweza kusababisha hasara kubwa za mali.
Hata hivyo, Morningstar post ilimtafuta Afisa Afya Halmashauri ya Mkurunga kuzungumzia athari za moto lakini hakuweza kupatikana licha ya juhudi za kumtafuta zinaendela.