NA MWANDISHI WETU

WANANCHI wa Kongowe, Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani wamelalalamikia uharibifu wa mazingira unaofanywa na Kiwanda cha vinywaji cha U – Fresh ambacho kinatiririsha maji machafu kwenda kwenye makazi yao na kwenye vyanzo vya maji.

Wakizungumza na MorningStarPost, wananchi hao wamesema suala hilo limekuwepo kwa muda mrefu, wametoa malalamiko yao sehemu mbalimbali, lakini Mamlaka zinazohusika zimeshindwa kuchukua hatua za kuwasaidia.

Walisema, maji hayo machafu kutoka kiwandani hapo yamekuwa yakitapakaa kwenye maeneo mbalimbali na kuingia kwenye bonde la maji ambalo wanalitegemea kwa shughuli zao zikiwemo za kilimo na ufugaji.

“Kuna wakati unapanda mimea inashindwa kustawi kutokana na maji hayo ambayo huenda yana kemikali hatari ambazo zinatuathiri na sisi bila kujua, vile vile kwenye bwawa tunalotumia kuna viumbe wakiwemo Samaki, nao wanakufa kwa wingi na hata wavuvi nao wapo hatarini,” alisema Juma Mustafa, mkazi wa Kongowe.

Mustafa alisema, hali hiyo inasababisha shughuli za kiuchumi kukwama kwani wapo wanaoishi kwa kutegemea kilimo na hata uvuvi kwenye bwawa ambalo lipo kwenye eneo hilo.

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Simon alisema, zipo taarifa kwamba baadhi ya watumishi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) wanajua kuhusu suala hilo, lakini hakuna hatua walizochukua na wengine wameligeuza kuwa mradi wa kujinufaisha kiuchumi.

“Ninavyofahamu viwanda vinatakiwa kuwa na mfumo wa kutibu maji machafu, lakini hapa sidhani kama wanao ndio maana maji yanazagaa hovyo, tumelalamika kwa muda mrefu hakuna hatua zozote zinazochukuliwa, ingawa yapo madai kwamba kuna Maafisa wa NEMC wamepewa chochote ili kufumbia macho suala hili,” alisema.

Alisema, wanashawishika kuamini hilo kwani licha ya kuwapo kwa taarifa ya Maafisa hao kufika kiwandani hapo na kukagua, bado maji machafu yanaendelea kutiririka na wananchi, mimea na viumbe hao wanaendelea kuathirika.

“Tunaiomba Serikali hususani Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira watusaidie, tumesikia wiki chache zilizopita Waziri husika amekifungia kiwanda, tunaomba aje na huku ili ashuhudie wananchi wake tunavyoteseka na ikimpendeza afanye maamuzi,” alisema Simon.

Alipotafutwa Meneja Uzalishaji wa Kiwanda hicho Cheng Cheng kwa ajili ya kuzungumzia madai hayo, alikiri na kusema Maafisa wa NEMC walifika kwenye eneo hilo na walipa wiki mbili bila maandishi na kumtaka arekebishe tatizo hilo, lakini MorningStarPost imeshuhudia maji machafu yakiendelea kutiririka.

“Ndugu mwandishi hapa kuna mambo ambayo yanafikirisha sana, tangu kiwanda kimeanzishwa ni miaka kadhaa sasa imepita, NEMC wanakuja wanakagua wanaondoka bila kuchukua hatua, Maafisa Afya wa Mkoa wa Pwani nao wanalifahamu hili tatizo na wanaonekana mara kwa mara wanaingia kiwandani na hawachukui hatua yoyote, unadhani hapo kuna nini kinaendelea?” alihoji mwananchi mwingine wa Kongowe.

Jitihada za kumpata Msemaji wa NEMC hazikufanikiwa, na mwandishi wa habari hizi anaendelea na jitihada za kuwasiliana na Waziri mwenye dhamana na Mazingira kwa ajili ya kufahamu kama ana taarifa kuhusu suala hilo na hatua ambazo zitachukuliwa kwa kiwanda hicho na kwa Maafisa wanaodaiwa ‘kuwalinda’ wenye kiwanda hicho.

Hata hivyo, taarifa zinaonyesha kuwa, kiwanda hicho kwa muda mrefu kimekuwa kikidaiwa kukiuka taratibu mbalimbali za uendeshaji na Kimazingira, ambapo mwaka 2014, kiliwahi kufungiwa na Shirika la Viwango (TBS) baada ya kubainika Juisi iliyokuwa inazalishwa na kiwanda hicho ilikuwa na vimelea vya wadudu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *