Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameuagiza uongozi mpya wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kujipanga kwa kufanya mageuzi ya kiutendaji na kitaaluma yatakayokiwezesha chuo hicho kuwa taasisi bora, imara na yenye ushindani.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipokutana na uongozi mpya wa chuo hicho uliofika Ikulu Zanzibar kupokea maelekezo baada ya kuteuliwa hivi karibuni.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuboresha usimamizi wa chuo, kuimarisha uwajibikaji, kusimamia ipasavyo mapato na matumizi ya fedha, kuendeleza miundombinu ya kisasa pamoja na kuimarisha ushirikiano na vyuo vya ndani na nje ya nchi ili kuinua ubora wa elimu, utafiti na ubunifu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la SUZA, Prof. Hemed Rashid Hikmany, ameahidi kuwa uongozi mpya utatekeleza maelekezo ya Serikali kwa lengo la kuifanya SUZA kuwa chuo bora na chenye ushindani wa kimataifa.