
Baadhi ya Madereva wa Bajaji maeneo ya Tegeta Kibaoni, jijini Dar es Salaam, wamelalamikia hospitali binafsi ya Kitengule kufanya uchafuzi wa mazingira unaohatarisha afya zao.
Madereva hao wamesema hospitali hiyo inatiririsha maji taka kwenye mifereji ya maji ya mvua barabarani na kuchoma taka za hospitali kusababisha moshi kutapakaa maeneo hayo na kuathiri afya zao.
Akizungumza na Morningstar post, Bw Fred Deogratus ambaye ni afisa habari wa umoja wa madereva wa Bajaji Kibaoni, alisema kero kubwa katika maeneo hayo ni mbili.
Alisema hospitali ya Kitengule imepitisha bomba za maji taka na kuyaelekeza kwenye mitaro ya maji ya mvua, hivyo imekuwa ni kero kubwa kwa wakazi na abiria wanaokuja kupanda usafiri wa bajaji.
“Kero nyingine inayotusumbua hapa ikifika saa tano usiku wanachoma taka za hospitali na moshi unasambaa maeneo yote hivyo, kusababishia kero sana, tunaomba watu wa mazingira waliangalie hili kwa kuwa limekuwa kero kubwa kwetu,” alisema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Wazo Bw. Medard Mashauri, alikiri kuzifahamu kero hizo na kuahidi kuzifanyia kazi.
Akijibu malalamiko hayo, Afisa Mazingira na Afya za Watu wa hospital hiyo Bw. William Mhemu, alisema hospitali hiyo inatumia mtambo wa kisasa wa kuchoma taka.
Bw. Mhemu alisema anashangazwa na malalamiko hayo ya wananchi kwa sababu mamlaka za serikali likiwemo Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira NEMC wanafanya ukaguzi katika hospitali hiyo mara kwa mara.
Aidha, kuhusu malalamiko ya kutiririsha maji taka kwenye mifereji ya maji ya mvua, Bw Muhemu alisema maji hayo yanayoonekana kwenye mifereji hayatoki kwenye hospitali yao yanatokea mbali, hivyo alitaka suala hilo liendelee kuchunguzwaa kubaini ukweli