Na Hassan Kimweri, WAF-Dar es Salaam

Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, amesema Tanzania imeendelea kuimarisha uwezo wa kujiandaa na kukabiliana na ugonjwa wa Ebola na dharura nyingine za afya kupitia ushirikiano wa karibu na Shirika la Afya Duniani (WHO), na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Akizungumza leo Juni 25,2026 Jijini Dar es salaam katika mkutano maalumu wa kujadili mwenendo wa mlipuko wa Ebola katika Kanda ya Afrika, Dkt. Magembe amesema magonjwa ya mlipuko hayatambui mipaka ya nchi, hivyo usalama wa afya ni jukumu la pamoja linalohitaji uratibu na ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

“Tanzania imekuwa ikiendelea kujiandaa tangu ugonjwa huu ulipotangazwa kuwa dharura ya Afya ya umma Duniani, ni kweli kuwa hadi sasa hatujapata kisa chochote nchini Tanzania, lakini maandalizi na utayari havianzi baada ya ugonjwa kugundulika nchini, huanza mapema kabla ya kisa chochote kutokea hiyo ndiyo sababu ya sisi kukutana hapa leo” amesema Dkt Magembe

Amesesitiza kuwa Tanzania inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya mlipuko wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo unaoendelea katika nchi jirani za DRC na Uganda kupitia mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, ushirikiano wa kuvuka mipaka na mikutano ya mara kwa mara ya kitaalamu.

Aidha amebainisha kuwa dharura za afya huathiri si sekta ya afya pekee bali pia uchumi na maendeleo ya jamii, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwekeza katika mifumo imara na himilivu ya afya yenye uwezo wa kuzuia, kugundua na kukabiliana kwa haraka na milipuko ya magonjwa.

Ameongeza kuwa mkutano huo umetoa fursa muhimu ya kupata taarifa za hivi karibuni kuhusu mwenendo wa ugonjwa huo, kutathmini vihatarishi vinavyojitokeza na kujifunza uzoefu kutoka maeneo yaliyoathirika ili kuimarisha zaidi hatua za maandalizi na mwitikio.

Katika hatua nyingine amewashukuru wadau wote wa maendeleo kwa mchango wao katika kuimarisha usalama wa afya nchini, akieleza kuwa ushirikiano huo umewezesha kufikiwa kwa maamuzi na hatua madhubuti zinazolenga kuilinda Tanzania na ukanda mzima dhidi ya tishio la Ebola na magonjwa mengine ya mlipuko

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *