WAKAZI wa Halmashauri ya Nyangh’wale ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakinufaika na miradi ya fedha za CSR kutoka mgodi wa Barrick Bulyanhulu,kipindi hiki tena wamefikiwa neema ya kupata fedha kiasi cha shilingi milioni 401 za mradi wa ‘Barrick-Twiga Future Forward Education Program, ambazo zitafanikisha kuboresha miundo mbinu  ya wanafunzi wa Kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari ya Serikali ya Nyang’hwale iliyopo mkoani Geita.

Hafla ya kuanza uwekezi wa jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza kutekelezwa kwa mradi huo utakaohusisha ujenzi wa mabweni 2, Vyumba vya madarasa 5 pamoja na vyoo  8 imefanyika katika shule hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa Meneja Mkazi wa Barrick nchini.Dk.Melkiory Ngido.

Katika hotuba aliyoitoa katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali,wananchi na wanafunzi, Dk.Ngido alisema  Barrick itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuchochea maendeleo ya jamii kupitia sekta mbalimbali, hususani sekta ya elimu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Alisema Barrick-Twiga inaamini kuwa elimu ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla na taifa lolote linalotaka kujenga uchumi imara, jamii yenye maarifa, na kizazi chenye ushindani, halina budi kuwekeza kwa makusudi katika elimu na ndio maana kampuni inaiona elimu siyo tu kama eneo la uwajibikaji kwa jamii, bali kama nguzo ya kimkakati ya maendeleo ya taifa.

“Tunafahamu kuwa darasa bora hujenga ufaulu bora. Bweni salama hujenga utulivu wa mwanafunzi. Mazingira safi ya usafi hulinda afya, heshima na hadhi ya mtoto wa Kitanzania. Hivyo basi, tunapojenga miundombinu ya elimu, tunakuwa tunajenga zaidi ya majengo; tunakuwa tunajenga ndoto, uwezo, fursa na maisha ya baadaye.”alisema.

Dk.Ngido alisema katika kuthibitisha dhamira hiyo, mwezi Machi mwaka 2023, Barrick iliahidi kutoa Dola za Marekani milioni 30 kuunga mkono ajenda ya Serikali ya Tanzania ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini. Kupitia mpango wa Barrick-Twiga Future Forward Education Programme, lengo ni kujenga madarasa 1,090, mabweni 270 na matundu ya vyoo 1,640 katika shule 161 nchini kote, zenye uwezo wa kuhudumia takribani wanafunzi 49,000 zitakapokamilika.

Alisema  katika awamu ya kwanza ya mpango huu, yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 10, ilianza Julai 2023 na kukamilika Desemba 2024, ambapo shule 64 zilinufaika kupitia ujenzi wa madarasa 396, mabweni 97 na vyoo 600.

Aidha, awamu ya pili, pia yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 10, ilianza Machi 2025, na kufikia Aprili 2026 ilikuwa imefikia zaidi ya asilimia 83 ya utekelezaji. Katika awamu hii, takribani shilingi bilioni 19 zimeshatolewa, sawa na asilimia 79 ya bajeti ya awamu hiyo, kwa ajili ya shule 65, zikiwemo madarasa 318, mabweni 116 na vyoo 542.

 “Katika utekelezaji wa awamu hii ya pili, Shule ya Sekondari Nyang’hwale ni miongoni mwa shule zinazopata manufaa ya moja kwa moja kupitia ushirikiano huu. Napenda kuweka bayana kuwa, kwa shule hii pekee, Barrick-Twiga imeshalipa shilingi 304,930,973, sawa na asilimia 76 ya fedha za mradi, kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matano, mabweni mawili na vyoo vinane”alisema Dk.Ngido..

 Akifafanua zaidi faida za Mradi huu katika jamii ya Nyanghwale alisema utawezesha na kuongeza nafasi za wanafunzi kujifunzia katika mazingira bora zaidi,kupunguza msongamano madarasani,kuimarisha mazingira ya malazi kwa wanafunzi, hususan wa kike na kuboresha usafi, afya na hadhi ya shule kwa ujumla.

Kwa upande wake , Katibu Tawala wa Halmashauri ya Nyang’hwale, Bw. Kaunga Amani amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira bora kwa wawekezaji wa nje na ndani ambao kupitia uwekezaji wanaendelea kuwanufaisha watanzania.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Ndg. Husna Toni ameishukuru Barrick Tanzania kwa mchango mkubwa uliowezesha ujenzi wa miundombinu hiyo ambao itasaidia kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi sambamba na kuwawezesha kusoma katika mazingira rafiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *