OWM-TAMISEMI
Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa imejipanga kudhibiti ukuaji holela wa miji kwa kuelekeza nguvu kubwa katika upangaji wa maeneo ya pembezoni kabla hayajajaa makazi yasiyo rasmi.
Akizungumza katika Jukwaa la 13 la Miji Duniani (WUF13), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema kupanga miji mapema ni njia bora ya kuepuka gharama kubwa za kurekebisha miundombinu baadaye.
“Kuweka miundombinu baada ya maeneo kujengwa holela ni gharama kubwa zaidi kuliko kuyapanga mapema,” amesema Prof. Shemdoe.
Amesema miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Arusha inaendelea kukua kwa kasi, hivyo Serikali imeanza kutumia teknolojia ya GIS, katika upangaji wa viwanja na kutumia miongozo mipya ya maendeleo ya miji ili kuhakikisha ukuaji huo unakuwa endelevu.
Prof. Shemdoe pia ametaja miradi ya TACTIC na DMDP kuwa sehemu ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika barabara, masoko, mifumo ya maji ya mvua na miundombinu inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.