▪️Asema kuna miradi inakwama utekelezaji sababu ya migawanyiko

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa waepuke migogoro na mizozo kwa sababu kuna miradi inakwama utekelezaji kutokana na migawanyiko.

“Twendeni tukatimize wajibu wetu, tuache migawanyiko kwa sababu hayo si matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesisitiza wakati akizungumza na washiriki wa Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) katika ukumbi wa mikutano wa AICC, jijini Arusha.

Ametoa wito huo Jumatano, Aprili 22, 2026 wakati akifungua mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo na kusisitiza kuwa waangalie uwezekano wa kuondoa uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti ambao hivi sasa unafanyika kila mwaka.

“Tuepuke migogoro, Waheshimiwa Mameya, Madiwani na Wenyeviti; kuna baadhi ya maeneo tunachelewa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa sababu ya migogoro inayotengeneza migawanyiko.”

“Ondoeni utaratibu wa kuchagua Makamu Mweneyekiti kila mwaka kwani jambo hili linaleta makovu. Nimeshamuagiza Waziri wa TAMISEMI amuandikie Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama ni sheria ifutwe, kama ni kanuni ibadilishwe, lakini kama mkutano huu una mamlaka, utaratibu wa kuchagua Makamu Mwenyekiti kila mwaka ufutwe,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema utaratibu wa sasa unawanyima fursa viongozi walioko madarakani kujielekeza kwenye masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi na badala yake wanajikuta kwenye harakati za kugawana vyeo.

“Wenyeviti wanajikuta wanaongoza watu waliogawanyika na hili halileti tija. Hivi sasa walioko madarakani bado wanajifunza kazi, tayari wengine wameshaanza kampeni kuwania nafasi zao,” amesisitiza.

Aidha, aliwataka viongozi watakaochaguliwa kesho wahakikishe wanakuwa chachu ya maendeleo na kusimamia maslahi ya wananchi kwa vitendo na kuongeza: “Kwa viongozi mtakaochaguliwa, mhakikishe mnakwenda kusaidia Jumuiya yetu na maslahi ya wananchi, muwe viongozi wanaopinga rushwa kwa vitendo. Mhakikishe mnakuwa daraja la kuleta maendeleo kwa wananchi na kuitafsiri Dira ya 2050.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *