Mwenyekiti wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 Jaji Chande Mohamed Othman amesema, vifo vilivyotokana na ghasia za uchaguzi huo ni 518.

Jaji Chande amesema hayo leo, Aprili 23, 2026 Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha ripoti ya tume hiyo, ambapo wanaume ni 490, sawa na asilimia 94.6 na wanawake ni 28, sawa na asilimia 5.4 na vingi kati vya vifo hivyo vilikuwa sio vya kawaida (unnatural).

Amesema, Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na vifo vingi zaidi, ukiwa na vifo 182, ikifuatiwa na Mkoa wa Mwanza vifo 90; Mbeya vifo 80; na Mkoa wa Arusha vifo 53.

Kati ya vifo hivyo 518, ishirini na moja (21) vilikua vya watoto. Katika kundi hilo, 15 walikuwa watoto wenye umri kati ya miaka 15 – 17, wanne (4) walikuwa na umri kati ya miaka 7 – 10, na wawili (2) umri chini ya miaka mitano.

“Vifo 502 sawa na asilimia 96.9 vilikuwa vya raia (civilians), na 16 sawa na asilimia 3.1 vilikuwa vya maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama.”

“Kati ya watu 518 waliofariki, 373 walifikishwa hospitali wakiwa wamefariki, majeruhi 121 walifariki wakati wakiwa wanapatiwa matibabu, na maiti 24 hakuna taarifa kutoka vituo vya kutolea huduma za afya. Kati ya Maiti 518, maiti 480 sawa na asilimia 92.7 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na familia,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *