Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa, amesema Serikali imefikia uamuzi wa kuijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya mchakato wa kina wa kitaalamu, akisisitiza kuwa mradi huo ni uwekezaji sahihi wenye manufaa mapana kwa taifa.
Akiwasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Aprili 22, 2026, jijini Dodoma, Mchengerwa amesema hatua hiyo inalenga kukidhi ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi nchini.
Amesema mjadala uliojitokeza kuhusu uamuzi wa kuijenga upya Muhimbili badala ya kujenga hospitali mpya eneo jingine ni wa msingi na unapaswa kuheshimiwa, lakini akaeleza kuwa historia inaonesha miradi mingi mikubwa ya maendeleo hupingwa mwanzoni lakini baadaye huleta manufaa makubwa kwa wananchi.
“Taifa linalouliza maswali ni taifa linalojitambua, na Serikali inayowajibika ni ile inayojibu kwa uwazi. Lakini pia uzoefu unaonesha kuwa miradi mikubwa ya kimkakati mara nyingi hupingwa mwanzoni, ila baadaye huonekana umuhimu wake,” amesema Mhe Mchengerwa.
Waziri ameeleza kuwa Muhimbili imekuwa na historia ya zaidi ya miaka 120 na kwa sasa inakabiliwa na changamoto za miundombinu chakavu, ongezeko la wagonjwa pamoja na mahitaji makubwa ya huduma za kisasa.
Akifafanua kuwa mwaka 2025 pekee hospitali hiyo ilihudumia wagonjwa zaidi ya 44,000 waliolazwa na zaidi ya 458,000 wa nje, huku ikiokoa takribani shilingi bilioni 96.8 ambazo zingetumika kwa rufaa za matibabu nje ya nchi.
Aidha, amesisitiza kuwa pamoja na umuhimu wa kujenga hospitali mpya, bado kuna ulazima wa kuendeleza Muhimbili kutokana na uwepo wa wataalamu zaidi ya 4,000 wenye utaalam wa juu ambao ni hazina kubwa ya taifa.
“Muhimbili si majengo tu, ni mkusanyiko wa utaalam, uzoefu na mifumo ya ubobezi ambayo imejengwa kwa muda mrefu. Hatuwezi kuacha msingi huo,” amesisitiza.
Kuhusu gharama, Mhe. Mchengerwa amesema mradi huo unakadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 468.5, huku akibainisha kuwa sehemu kubwa ya mchango wa Serikali si fedha taslimu bali ni msamaha wa kodi kwenye vifaa vya mradi.
Ameongeza kuwa uchambuzi wa kimataifa unaonesha Tanzania inalipa gharama nafuu ya takribani dola 1,819 kwa mita ya mraba, kiwango ambacho ni cha chini ikilinganishwa na nchi nyingi duniani.
Aidha, mradi huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wengi zaidi, kuongeza idara za ubingwa bobezi kutoka 13 hadi 33, pamoja na kuongeza vitanda hadi zaidi ya 2,800.