NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya ulinzi ya HUAYUAN, iliyopo Mtaa wa Serengeti, Mikocheni jijini Dar es Salaam, inadaiwa kutozingatia usalama wa wafanyakazi wake kwa kuwapatia vitendea kazi vinavyohatarisha maisha yao.
Kampuni hiyo, ambayo inamilikiwa na raia wa China kwa kushirikiana na baadhi ya vigogo ambao ni raia wa Tanzania, inadaiwa kusababisha madhara kwa wafanyakazi wake kadhaa ambao wengine kwasasa wapo majumbani wakiuguza majeraha makubwa baada ya kuumia wakiwa kazini.
Mmoja wa wafanyakazi hao, Fabiano Yohana, alipata ajali mbaya ya pikipiki Septemba 22, 2025 na kuvunjika mguu, ambapo alipelekwa hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa ajili ya huduma ya kwanza na baadae alihamishiwa Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Taarifa zaidi zinadai kwamba, wafanyakazi hao licha ya kulalamika mara kadhaa kwa uongozi ili wanununuliwe vitendea kazi vipya, lakini hakuna utekelezaji unaofanyika na badala yake wanalazimishwa kuendelea kutimiza majukumu yao kwa vitendo kazi vilivyopo ambavyo ni vibovu na hatari kwa maisha yao.
“Wao wanachoangalia ni kazi zao tu, lakini hawajali wanaozifanya hizo kazi, hapa kila siku watu wanaumia kutokana na mazingira magumu ya kazi, lakini mabosi hawajali kabisa, tunaziomba mamlaka zinazohusika na usalama wafanyakazi waje kukagua hii kampuni wajiridhishe kama kweli inafuata taratibu, nadhani watakutana na madudu mengi sana,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe.
Alisema, haya yanayozungumzwa ni machache, yapo mengi ambayo atayatoa kwa waandishi wa mtandao huu ili yafanyiwe kazi na hatua zichukuliwe kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi.
Alisema, mbali na vitendeakazi hivyo ambavyo ni pikipiki, hawana vifaa vya kulinda usalama wao, huku akimtaja mmoja walinzi ambaye aliumia kutokana na kuangukiwa na chuma akiwa kwenye ulinzi.
“Kuna mambo mengi sana hapa ndugu mwandishi na nitakueleza yote ili muandike mamlaka zinazohusika zichukue hatua, maana hawa jamaa wanakiuka taratibu nyingi sana na wanafanya vitendo ambavyo naamini Serikali ikivijua hawawezi kuwafumbia macho,” alisema.
Aidha, mfanyakazi huyo alimkabidhi mwandishi wetu ushahidi wa tuhuma nyingine mbalimbali, sambamba na majina na picha za wafanyakazi wote ambao wameumia wakiwa kazi kutokana na vitendea kazi duni, ambapo MorningStarPost itaendelea kuziandika mfululizo sambamba na habari nyingine ambazo tayari uchunguzi wake umekamilika.