Na Anania Makumba
KAMPUNI ya HUAYUAN inayojihusisha na shughuli za ulinzi, inalalamikiwa na wafanyakazi wake kwa kuendesha shughuli zake bila kufuata sheria za ajira na kusababisha madhara makubwa wakiwa kazini.
Kampuni hiyo ambayo ipo Mtaa wa Serengeti, Mikocheni, jijini Dar es Salaam, inamilikiwa na raia wa China kwa kushirikiana na Mtanzania ambaye amewahi kushika moja ya nafasi kubwa nchini (jina tunalihifadhi kwasasa).
Wakizungumza na mwandishi wetu kwa sharti la kutotajwa majina yao, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo walisema, kutokana na vitendea kazi duni na kutozingatiwa kwa usalama wakiwa kazini, wamejikuta wakiumia na kibaya zaidi kampuni inashindwa kuwahudumia.
Mmoja wa wafanyakazi hao alisema, wanapopata matatizo ikiwemo kuumia wakiwa kazini, hawapati huduma zinazostahili na wakilalamika, wanatishiwa kufukuzwa kazi.
“Kuna pikipiki tunakabidhiwa kwa ajili ya shughuli zetu za kazi, lakini pikipiki hizo ni mbovu sana, zimekuwa chanzo cha wengi kupata ajali, na hata wanapopata ajali hakuna anayejali, ukijaribu kulalamika unatishiwa kufukuzwa kazi hata kama mtu ana madai ya msingi,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Alisema, raia hao wa Wachina wamekuwa wakifanya vitendo hivyo kwa kile wanachoamini hakuna anayeweza kuwafanya chochote kwasababu ya vigogo ambao wanashirikiana nao kwenye kampuni hiyo.
Aidha, wafanyakazi hao waliwataja raia wanne wa China (majina yao tunayo), ambao wanafanyakazi ambazo zingeweza kufanywa na wazawa, jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi zinazolinda ajira za watanzania.
“Tunanyanyaswa sana na hatuna pa kukimbilia na ajira ni ngumu tunaona bora tukomae hapa hapa, tunaiomba serikali itupie jicho kampuni hii ili irekebishe haya mambo tufanye kazi kwa kuzingatia sheria zilizopo zinazolinda afya zetu,” alisema mfanyakazi mwingine.
Mwandishi wa Habari hizi alimtafuta Afisa Rasilimali watu wa kampuni hiyo, hata hivyo hakuwa tayari kujitu tuhuma hizo kwa madai kwamba sio Msemaji wa Kampuni ambapo aliongea kwa kifupi “bosi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu yupo nje ya nchi, hivyo tunaomba mawasiliano yenu, akirudi tu tutawajulisha.”
Hata hivyo, tangu wakati huo ambapo ni siku kadhaa zimepita, uongozi wa kampuni hiyo haujawasiliana na mwandishi wetu kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa madai hayo, ingawa jitihada za kuwasiliana na mamlaka nyingine zinazohusu ajira zinaendelea.
MorningStarPost siku chache zijazo, baada ya kupata kauli ya Mamlaka za ajira, itatoa habari hii kwa undani zaidi ikiwemo kuweka ushahidi wa picha za waliopata ajali na kutelekezwa sambamba na raia wa kigeni wanaofanya kazi ambazo hawaruhusiwi na tuhuma nyingine zinazoikabili kampuni hiyo.