Na Angela Msimbira – OR-TAMISEMI
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Bi. Janet Mayanja, ametoa wito kwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya Mfumo wa Tausi ili kuongeza uelewa, kuimarisha uwajibikaji na kukuza ushirikiano kati ya Serikali na wananchi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la Ofisi ya Rais – TAMISEMI katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika katika viwanja vya Nzuguni, Mkoani Dodoma, Bi. Janet amesema bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa wananchi kuhusu mfumo huo mpya wa kidijitali.
“Ni muhimu wananchi wakaelewa dhima ya mfumo huu na namna unavyoweza kuwawezesha kupata huduma kwa haraka, uwazi na kwa ufanisi mkubwa zaidi,” amesisitiza Bi. Janet.
Ameongeza kuwa elimu endelevu kwa umma ni muhimu ili kuhakikisha mfumo wa Tausi unatekelezwa kikamilifu na kwa mafanikio, hasa katika ngazi ya Serikali za Mitaa.
Mfumo wa Tausi ni jukwaa la kidijitali linalolenga kuboresha uratibu wa taarifa, utoaji wa huduma na kuongeza uwajibikaji katika utendaji kazi wa Serikali za Mitaa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.