WANANCHI wa Mabibo jijini Dar es Salaam na maeneo ya jirani, hivi karibuni walijikuta kwenye taharuki baada ya kile kinachoelezwa ni kuharibika kwa moja ya mitambo ya Kiwanda cha Royal Soap & Detergent na kusambaza kemikali zinazodaiwa ni hatari.
Tukio hilo lilitokea Februari 17, 2025 majira ya jioni, ambapo inaelezwa ‘valve’ kwenye ‘Sulfornation Plant,’ ilifyatuka na hivyo iliwalazimu wafanyakazi wa kiwanda hicho wazime mtambo huo ili kuepusha madhara makubwa zaidi ambayo yangetokea.

Inaelezwa, tukio hilo limesababisha madhara kwa wananchi wengi wanaoishi jirani na kiwanda hicho, sambamba na baadhi ya wafanyakazi akiwemo Mlinzi wa Kampuni ya NK Security aliyetajwa kwa jina la Fadhila Yahya.
Wakizungumza na MorningStar Post , baadhi ya mashuhuda walisema, walipatwa na taharuki baada ya kusambaa kwa hewa ambayo ilisababisha watu wengi kukohoa na kupata maumivu makali ya macho.
“Tulishangaa kuna kitu kama wingu hivi limetanda, watu wakaanza kukohoa na kupata maumivu makali sana ya macho, baadae tukasikia kwamba kuna kifaa kwenye mtambo wa kiwanda cha sabuni kimefyatuka, kwa kweli tulipata wakati mgumu sana,” alisema mkazi wa Mabibo, aliyejitambulisha kwa jina moja la John.
Alisema, kilichowatisha zaidi ni baada ya kusikia mlinzi wa kampuni inayolinda kiwanda hicho amekimbizwa hospitali, jambo ambalo liliongeza taharuki zaidi na wakahisi wanaweza kupata madhara makubwa na hivyo wakaanza kukimbia hovyo.
Akizungumza kiwandani hapo, mmoja wa maafisa wa kiwanda hicho Shalanda Shalanda, alikiri kutokea kwa tukio hilo, ambapo alisema ni mara ya kwanza kutokea tangu kiwanda hicho kilipoanzishwa.
Kwa upande wake mmoja wa maafisa wa kampuni ya NK Security Juma Ongoa alikiri mlinzi wao kupata madhara kutokana na tukio hilo, ingawa alisema anaendelea vizuri.
Hata hivyo, uchunguzi zaidi uliofanywa na MorningStar Post umebaini kuwa, tukio hilo halijaripotiwa polisi, huku kukiwa na malalamiko mengi ya kiwanda hicho ambacho kipo chini ya Mohamed Enterprises Limited (MeTL).
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, kusambaa kwa vitu vinavyodaiwa ni kemikali sio mara ya kwanza, ambapo tangu mwaka 2013 kiwanda hicho kimekuwa kikilalamikiwa na wananchi, licha ya Serikali kuagiza mara kadhaa kurekebisha miundombinu yake.
Mwaka 2021, aliyekuwa Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Suleiman Jafo alitoa siku 45 kwa uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha wanazuia kusambaa kwa hewa hiyo, ingawa bado hali ni mbaya.
Wananchi hao walidai kwamba, wamekuwa wakivuta hewa inayohisiwa ni kemikali, ingawa mara kadhaa wahusika wamekuwa wakidai ni sabuni ya unga, pia mwaka 2016, kiliwahi kutozwa faini ya Shilingi Milioni 10 na Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kutiririsha maji machafu yenye sumu.
“Tunaziomba Mamlaka zinazohusika hususani NEMC zitusaidie, kwa miaka yote hii tumekuwa tukivuta hewa chafu, na kubwa zaidi ni hili tukio la hivi karibuni ambalo limetupa mashaka makubwa sana na huenda tumeathirika kiafya,”
Tunaomba ikiwezekana ufanyike uchunguzi wa afya zetu ili tujue kama tupo salama au tumeshaathirika na hizi kemikali tunazovuta kila siku,” alisema mwananchi wa Mabibo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.