Waziri Maji Jumaa Aweso

Na Mwandishi Wetu

MRADI mkubwa wa ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya usambazaji wa maji kwenye Kijiji Cha Soliwaya Wilayani Wanging’ombe, Mkoani Njombe kwa ufadhili wa Serikali ya India, unadaiwa kutekelezwa chini ya kiwango.

Mradi huo ambao unafadhiliwa na Serikali ya India, ambao mshauri mwelekezi ni kampuni ya WAPSCO, ulikabidhiwa kwa kampuni ya Lasern and Toubro (LNT) ya Upanga jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na kampuni ya Earth Tecnochon Private Limited (EPTL).

Kwa mujibu wa chanzo kilichopo ndani ya moja ya makampuni yanayotekeleza mradi huo kinadai, kutokana na kukosa usimamizi mzuri, imechangia kwa kiasi kikubwa kutekelezwa chini ya kiwango.

Chanzo hicho ambacho kiliomba jina lake lisitoke hadharani kilisema, uwekezekano wa mradi huo kudumu kwa miaka mingi ni mdogo, kutokana na kutozingatiwa kwa manunuzi na matumizi sahihi ya vifaa kwenye ujenzi wa miundombinu hiyo.

“Hapa kinachofanyika ni bora liende tu, vifaa vinavyonunuliwa haviendani na maelekezo ya kitaalamu, kwa mfano nondo zinazohitajika ni 25 mm, lakini hapa zinawekwa za 20mm kwenye kitako cha kisima, jambo ambalo ni hatari kwa mradi huu, hauwezi kudumu kama ulivyotarajiwa,” kilisema chanzo hicho.

Aidha, mbali na hilo inadaiwa, wafanyakazi ambao wanatekeleza mradi huo wakiwemo mafundi, wanacheleweshewa malipo yao na usalama wa kazi haujazingatiwa, unaosababisha ufanisi kuwa mdogo na ni kinyume na mikataba ya kazi ya Kimataifa na Kitaifa.

“Huu ni mradi mkubwa ambao umefadhiliwa kwa fedha nyingi, lakini utekelezaji wake hauonyeshi kama unahusisha kiasi kikubwa cha fedha, wafanyakazi wanacheleweshewa malipo yao, pia usalama wao wakiwa kazini haujazingatiwa, ni wazi ikitokea mmoja wao amepata tatizo ikiwemo kuumia akiwa kazini, hakuna msaada wowote atakaoupata, kwa kuwa hata mikataba ya kazi hawana” kilisema chanzo hicho.

Mbali na hilo, chanzo hicho kilidai kwamba, wafanyakazi hao mbali na kufanyakazi kwenye mazingira magumu, hawana uhakika na maisha yao baada ya kumaliza mikataba yao na kampuni inayosimamia mradi huo, kwani hajaunganishwa na mifuko ya hifadhi ya Jamii.

“Hapa hakuna hata mmoja mwenye uhakika na maisha yake ya baadae, maana hakuna aliyejiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo NSSF, kwa hiyo wakimaliza mikataba yao wanarudi mtaani kuhangaika na maisha wakiwa hawana chochote.”

Uchunguzi zaidi kuhusu mradi huo kupitia vyanzo mbalimbali, umebaini kuwa, hakuna mkataba wowote unaoonyesha makubaliano ya kampuni zinazotekeleza mradi huo na haujasajiliwa kwenye mamlaka zinazohusika.

Pia, kampuni husika zinadaiwa hazifuati taratibu ikiwemo kulipa kodi zinazotakiwa na hata malipo kwa ajili ya manunuzi ya vifaa na kuwalipa wafanyakazi, yanatumwa moja kwa moja kutoka nchini India na kuingia kwenye akaunti binafsi ya mmoja wa wasimamizi wa mradi huo, badala ya kupitia kwenye akaunti ya kampuni jambo ambalo ni kinyume na sheria za fedha za kimataifa.

“Kuna mambo mengi sana hapa yanatakiwa kuchunguzwa lkiwemo suala la kodi, hawa jamaa nina uhakika hawalipi kodi inavyotakiwa na wanakiuka mambo mengi ikiwemo suala la utumaji wa fedha za utekelezaji wa mradi, kwa ufupi mradi huu unatekelezwa kienyeji mno,” kilisema chanzo hicho na kuelezea hofu ya kuwepo kwa utakatishaji wa fedha kupitia mradi huo, ambapo waandishi wetu wanaendelea kufuatilia madai hayo.

Walipotafutwa watendaji wanaosimamia kampuni zinazotekeleza mradi huo akiwemo Mkurugenzi wa EPTL aliyetambulika kwa jina moja la Montu ambaye yupo nchini India, alikiri kuwepo kwa changamoto kwenye mradi huo, ingawa alikwepa kujibu maswali mengi yenye utata kuhusu mradi huo.

Hata hivyo, Morningstarpost inaendelea kufuatilia zaidi kuhusu mradi huo kwenye mamlaka za serikali na ubalozi wa India, ambapo jitihada za kumpata Waziri wa Maji hazikufanikiwa na inaelezwa yupo nje ya nchi kwa shughuli za kiserikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *