Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dorothy Gwajima.

Na Mwandishi Wetu, Moshi

DIWANI mmoja mstaafu katika Halmashauri ya Mji wa Moshi anachunguzwa kutokana na tuhuma za kumbaka binti yake.

Waziri wa Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dorothy Gwajima sasa amebebeshwa zigo la Diwani huyo mstaafu anayedaiwa kumbaka binti yake huyo wa kumzaa.
Habari ambazo zimetufikia zinasema Waziri Gwajima ameagiza ofisi.yake kushughulikia suala la binti huyo ambaye amelalamika kwamba baba yake huyo mzazi amemwingilia kimwili bila idhini yake.
Mwezi Desemba mwaka jana binti huyo mwenye umri wa miaka 13 (jina lake tunalihifadhi) alilazimika kuondoka nyumbani kwa baba yake mjini Moshi na kukimbilia Kijiji kwa bibi yake mzaa mama wilayani Rombo mkoani humo Kilimanjaro kufuatia kile alichosema ni unyanyasaji wa kingono unaofanywa na baba yake.
Baadaye kwa usalama wake, binti huyo aliyekuwa anasoma darasa la saba alikimbilia jijini Dar es Salaam kwa ndugu wengine wa mama yake ambako alipewa msaada wa kisheria ikiwa ni pamoja na kufungua malalamiko kwenye Idara ya Ustawi wa Jamii na baadaye kufanyiwa vipimo hospitalini.
Katika maelezo yake binti huyo amesema baba yake amekuwa akimwingilia mara kwa mara na alipoona mambo yamezidi ameamua kukimbia.
“Nililalamika kwa mkewe ambaye ni mama yangu wa kambo akaniambia kwamba kama unajilegeza unategemea nini? Yaani badala ya kunisaidia akawa anamtetea baba. Nikajua sina mtetezi hapa na kuamua kuondoka”, amesema mtoto huyo.
“Kabla ya kukimbilia kijijini nilikwenda kwa mama mkubwa eneo la Himo ambaye alinishauri kwamba kwa usalama wangu na wake lazima nikajifiche Rombo kwasababu baba ana pesa na ni maarufu. Nilipokwenda kijijini bibi na mama mzazi walinishauri nikajifiche Dar es Salaam kwasababu baba alikuwa ananisaka Moshi nzima”, alisema.
Anasema baba yake na mama yake walitengana wakati akiwa mdogo, na kwamba yeye na wadogo zake pacha wawili walibaki kwa baba yao ambaye alioa mke mwingine na mama yake naye aliolewa na mume mwingine.
“Tumekuwa tukiishi bila matatizo yoyote na baba alikuwa ananilipia shule binafsi na wadogo zangu, pamoja na kaka yetu mwingine ambaye baba alimzaa na Mama yangu mkubwa kabla hajamuoa mama”, anasema.
Kwa maelezo ya binti huyo, kabla yeye na wadogo zake hawajazaliwa, baba yake alikuwa akihusiana kimapenzi na dada wa mama yake na wakapata mtoto mmoja wa kiume anayesoma kidato cha nne sasa.
“Kaka yetu (anamtaja jina) ni mtoto wa mama yetu mkubwa, baba mmoja mama mmoja na mama yangu. Yaani baba alianza kuzaa na mama mkubwa walipoachana akamtafuta mama wakahusiana tukazaliwa sisi”, amesema.
Binti huyo amehitimu darasa la Saba na sasa anasoma Kidato cha Kwanza kwenye shule moja ya sekondari wilayani Rombo, badala ya shule aliyopangiwa awali katika Halmashauri ya Mji wa Moshi kutokana na kile familia ilichosema ni sababu za kiusalama.
Alipoulizwa kwa simu, Diwani huyo mstaafu kupitia Chama kimoja cha upinzani alijibu kwa ukali: “Kama natembea na Mwanangu, unataka umuoe wewe?” kisha akakata simu.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, alipoulizwa kama anafahamu jambo hilo amesema binti anayelalamika anatakiwa afike ofisini kwake ili wapate maelezo ya kutosha kuhusiana na Binti huyo, ingawa Waziri Gwajima amewaelekeza familia ya binti huyo wawasiliane na maofisa wake wizarani kwa hatua zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *