NA MWANDISHI WETU

WAKAZI wa Mtaa wa Jogoo, Mbezi juu Wilayani Kinondoni, Dar es Salaaam wamekilalamikia Kiwanda cha kutengeneza zege kinachojulikana kwa jina la Dalin kwa kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira

Wakizungumza na Morningstar Post kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema, wanahofia huenda wakapata magonjwa kutokana na vumbi kali linalotoka kwenye kiwanda hicho kinachodaiwa kinamilikiwa na raia wa China na kusambaa kwenye makazi yao.

Pia, wananchi hao wamesema, kiwanda hicho kinatiririsha maji machafu ambayo wanahisi huenda yana kemikali ambazo zimeambatana na saruji na kusambaa mitaani na kuingia kwenye mifereji inayopitisha maji wakati wa mvua.

Walisema, wamesikia serikali imetangaza ujio wa mvua kubwa za Elinino, wanahofia kukumbwa na mafuriko kutokana na kuziba kwa mifereji hiyo na wameziomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kabla madhara hayajawa makubwa.

Aidha, walisema wanaamini kwamba kiwanda hicho hakikufuata taratibu zinazotakiwa kudhibiti uchafuzi wa mazingira, ndio maana kunajitokeza changamoto nyingi ikiwemo kusambaa kwa vumbi kali.

Morningstar Post ilimtafuta Msemaji wa kiwanda hicho ili kuzumgumzia malalamiko hayo ya wananchi, lakini hakupatikana na jitihada za kumtafuta zinaendelea.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Jogoo Raymond Kalyalya, alipotafutwa hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo, ambapo waandishi wetu pia wanaendelea kutafuta majibu kutoka kwenye mamlaka nyingine za Serikali zinazosimamia mazingira na taratibu za uendeshaji wa viwanda nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *