Na.OWM-TAMISEMI

Mkoa wa Kilimanjaro umeendelea kujidhihirisha kuwa moja ya nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania baada ya kuangazwa kwa mafanikio makubwa katika maadhimisho ya Siku ya Kilimanjaro yaliyofanyika leo katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere (Sabasaba), jijini Dar es Salaam. Mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri anayeshughulikia masuala ya Afya, Mhe. Jaffar Seif, ambaye alisema mkoa huo umebeba sura ya Tanzania duniani kupitia utalii, biashara, utamaduni na mchango wake katika maendeleo ya jamii.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Seif amesema Mlima Kilimanjaro si kivutio cha utalii pekee bali ni alama ya Taifa inayovutia maelfu ya wageni kila mwaka na kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa. Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia kampeni za utalii.

Aidha, Mhe. Dkt.Seif ametaka wananchi na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira na rasilimali za asili zinazobeba sekta ya utalii, akieleza kuwa utunzaji wa misitu, vyanzo vya maji na wanyamapori ni msingi wa kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi.

Maadhimisho hayo yalipambwa na maonesho ya bidhaa mbalimbali za Kilimanjaro, vyakula vya asili, sanaa za utamaduni na fursa za uwekezaji zilizovutia idadi kubwa ya wananchi waliotembelea banda la mkoa huo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *