Ikiwa ni sehemu ya kuimarisha diplomasia ya michezo, Humphrey Polepole Balozi na Mkuu wa Kituo cha Uwakilishi cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Cuba amekuwa na mazungumzo na Prof. Silvano Merced Len Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Michezo na Utamaduni – Manuel Fajardo.
Mazungumzo haya yalikuwa na lengo la kukamilisha mchakato wa kuanzisha mahusiano baina ya Chuo Kikuu cha Manuel Fajardo na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Mallya Tanzania.
Mpango wa muda mfupi ni kubadilishana waalimu wa Michezo katika maeneo ambayo yatakubaliwa na lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa mafunzo ya kimichezo nchini na tukitumia uzoefu wa Nchi ya Cuba.
Awali, Balozi Polepole amekutana na kufanya mazungumzo na Prof. Rolando V. Ortega Álvarez Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sanaa Cuba “Instituto Superior de Arte” (ISA), kukamilika kwa mazungumzo haya kwa mafanikio yanawezesha Taasisi yetu ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kushirikiana na ISA moja kwa moja katika kukuza Sanaa na Utamaduni na lengo la Serikali ikiwa ni kuwezesha tafiti za sanaa na utamaduni na kutengeneza mashirikiano yatakayowezesha muunganiko wa sanaa na utamaduni kati ya Africa na Amerika Latina.
Inaelezwa, January 2025, Mikataba mbalimbali ya Kisekta na Kitaasisi inatarajia kusainiwa Jijini Havana ikiwemo ya Taasisi hizi za Utamaduni, Sanaa na Michezo.