Na Mwandishi Wetu
Watumiaji wa vyombo vya moto vinavyotumia gesi wameonesha masikitiko yao juu ya usumbufu wanaopata wakati wa kuweka gesi kwenye vyombo vyao.
Solomon Albert, dereva wa bajaji anayetumia gesi amesema Oktoba Mosi, 2024 alitumia zaidi ya saa sita kusubiri nishati hiyo kutokana na foleni.
“Tatizo vituo ni vichache tulikuwa na vituo vitatu, kituo cha TAQA Dalbin kimepata hitilafu, sasa tuna vituo viwili vimebaki ambavyo navyo vimelemewa, ni muhimu Serikali ikaangalia namna ya kutengeneza mazingira kuvutia sekta binafsi kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo, kutuepushia adha hii ya kupoteza muda,” amesema.
Amesema bajaji yake ameichukua kwa mkopo na anapaswa kurejesha Sh40,000 kila siku lakini imekuwa vigumu kutokana na muda anaoupoteza kusubiri kujaza gesi.