Na Mwandishi Wetu

Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Tawi la Ilala jijini Dar es Salaam, wameingia kwenye kashfa baada ya fedha zilizotolewa na CCM Makao Makuu kukarabati jengo la ukumbi wa ofisi tawi la Ilala kutumika kinyume na zilivyokusudiwa, Morningstar POST imebainika.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Morningstar POST, fedha zilizotolewa na CCM Makao Makuu kiasi cha shilingi milioni tano kwa ajili ya ujenzi wa ukumbi wa jengo la CCM tawi la Ilala hazikutumika kama ilivyokusudiwa na chama.

Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya CCM tawi la Ilala, zinasema kuwa msaada wa ukarabati wa ujenzi wa ukumbi zilinunuliwa bomba kumi na mbili za chuma ambazo mpaka leo hazijatumika.

Taarifa zinasema kuwa baada ya viongozi hao kupata fedha hizo kutoka Makao Makuu ya CCM walinunua bomba kwa ajili ya ukarabati wa ukumbi wa jengo la CCM tawi la Ilala ambazo zilihifadhiwa ukumbini hapo kwa muda mrefu hadi walipoamua kuzipeleka kuhifadhi kwa diwani wa kata hiyo nyumbani kwake.

Mtoa taarifa hizi anadai kuwa mabomba ya chuma yaliotumika kama nguzo hayakuzidi mabomba manne mengine sita ndio yaliopelekwa kuhifadhiwa kwa diwani.

Wakereketwa na wadau wa maendeleo kwenye tawi hilo, wanahoji kuwa bomba kumi na mbili ndio zenye thamani ya shilingi milioni tano na mpaka sasa ukarabati wa ukumbi huo bado haujakamilika na vyoo vya ukumbi huo vinanuka na mapaa ya jengo hilo yameharibika.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa CCM tawi la Ilala, Antony  Kivugo, alikiri kuwa fedha hizo zilitolewa na kununuliwa mabomba ya nguzo kwa ajili ya kukarabati ukumbi huo, lakini kipindi hicho hakuwa katika uongozi.

Alisema kuwa alikuta mabomba nane yakiwa yamehifadhiwa katika ukumbi huo lakini kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda mabomba hayo yalikuwa yanapungua yakabaki sita hivyo walichukua jukumu la kuyapeleka kwa diwani wa kata hivyo kuyahifadhi.

“Ni kweli mabomba hayo yalikuwepo hapa…..lakini kupindi hicho mimi sikuwa kiongozi na nilipochukua uongozi sikuwahi kukabidhiwa mabomba hayo,” alisema Kivugo.

Aidha, wanachama na wakereketwa wa maendeleo wa tawi hilo, wamesema tawi hilo limejaa miradi lakini fedha zinazotokana na miradi hiyo nyingi zinaishia kwenye matumbo ya watu wachache na kusababisha mazingira ya jengo la tawi hilo kuwa katika mazingira machafu.

“Tunashangaa kuwa hata viongozi wakifanya ziara hapa viongozi wa tawi hili hawawaambi ukweli kuhusu jambo hili, wanatupiana mpira,” walisema bila kutaja majina yao.

Pia, wameiomba uongozi wa juu wa CCM kufuatilia ufisadi huu ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria ili kuimarisha chama.

Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Ilala, Saad Khimji alipotafutwa kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizi hakuweza kupatikana mara moja kupitia simu yake ya mkononi, juhudi zinaendelea kumpata ili kuzungumzia jambo hili.

Ofisi ya Tawi la CCM Ilala

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *