Na Mwandishi Wetu
Meneja wa Casino moja maarufu iliyoko maeneo ya Posta katikati ya jiji la Dar es Salaam, aliyefahamika kwa jina la Ergun, amekuwa akifanya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake wanaofanya kazi katika Casino hiyo.
Meneja huyo ambaye ni raia wa Uturuki, anafanya vitendo vya unyanyasaji, udhalilishaji na uonevu (sexual harassment) kwa wanawake kwa kutumia nafasi yake ya kazi.
Casino hiyo ambayo iko kwenye hoteli maarufu zamani ilikuwa inafahamika kama New Africa, wafanyakazi wa kike hawaajiriwi mpaka watoe rushwa ya ngono.
Kwa mujibu wa wafanyakazi wa Casino hiyo, ambao hawakutaka kutaja majina yao wamesema, meneja huyo ana lugha chafu kwa wafanyakazi, na anawataka wafanyakazi wa kike kimapenzi na wakimkataa anatafuta sababu za kuwafukuza kazi.
“Kila mfanyakazi anayekuja kufanya kazi katika Casino ile anatakwa kimapenzi na akikataa hapati kazi….mimi niliingia pale kwa kupitia njia nyingine lakini nilipotakiwa kimapenzi nilikataa….akanitafutia sababu ya kunifukuza”, alisema mmoja wa wafanyakazi.
Aliongeza kuwa baada ya kumkataa alimtafutia sababu kwa kumwahamisha nafasi yake ya kazi kutoka mapokezi na kumpeleka kuosha vyombo jikoni nafasi ambayo aliikataa kuendelea nayo akaacha kazi bila kupenda.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Morningstar POST, meneja huyo amesababisha mfanyakazi wa Casino hiyo, aliyefahamika kwa jina la Antonio January kuacha kazi baada ya kumwamisha nafasi yake ya kazi kutoka mapokezi na kumpeleka kuosha vyombo jikoni.
Mfanyakazi mwingine anayedaiwa kunyanyaswa kijinsia na kuachishwa kazi na meneja huyo ni Ntalia Uyango ambaye alihamishwa nafasi yake ya kazi kutoka mhudumu na kupelekwa kusafisha vyoo na baada ya mkataba wake kuisha akaachishwa kazi.
Wafanyakazi wa Casino hiyo wanasema meneja huyo akikutaka kimapenzi ukakataa lazima atakutafutia sababu na kukuondoa kazini.
Morningstar POST ilimtafuta meneja huyo ofisini kwake hakuweza kupatikana kwa kuwa alikuwa mapumnzikoni lakini alipopigiwa simu kupitia namba yake ya mkononi hakuweza kuzungumza lolote.
Hata baada kuandikiwa ujumbe kupitia simu yake ya whatsapp kuhusu tuhuma hizo hakujibu lolote licha ya kuonekana kupata taarifa alizoulizwa.
Afisa Rasilimali Watu wa Africa Princess Casino, aliyefahamika kwa jina la Vero alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi ndani ya Casino hiyo taarifa za unyanyasaji wa kijinsi zinazofanywa kwenye Casino hiyo alijibu kwa dharau na majigambo.
“Kwa kifupi…hatujapokea malalamiko yoyote au madai yoyote ya unyanyasaji wa ngono…….mwambie …….afuate taratibu za kisheria au atafute mwanasheria hatuwezi kuzungumza lolote kwaherini,” Vero alijitapa na kuondoka.
Kwa mujibu wa uchunguzi Casino hiyo mtendaji mkuu ni bwana mmoja anayefahamika kwa jina la Ali ambaye hata hivyo hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia taarifa hizi.
Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Nchini, (GBT), Bw. Daniel Ole Sumayan ameiambia Morningstar POST kuwa ni kosa kisheria mtu yeyote awe Mtanzania au mgeni kutoka nje ya nchi kufanya aina yoyote ya unyanyasaji wa kijinsia.
Alisema kuwa Casino ni sehemu ambayo kinachotakiwa kufanyika ni biashara ya michezo ya kubahatisha tu na sio vinginevyo.
Bw. Sumyan ameahidi kuchunguza na kufuatilia taarifa hizo za unyanyasaji wa wanawake kwenye Casino hiyo na kuchukua hatua stahiki za kisheria.
Aidha, amewataka wafanyakazi wote wa kwenye Casino iwapo wataona kuna aina yoyote ya udhalilishaji wafike kutoa taarifa kwenye bodi yake kwani wanahusika moja kwa moja kulinda na kusimamia haki za watu wote wanaendesha michezo hiyo.
“Watu wanaoendesha michezo hii wanatakiwa kuwa ni watu safi kwa mujibu sheria”, alisema Bw Sumayan
Morningstar POST inaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu suala hilo
Meneja wa Africa Princess Casino Bw. Ergun.