Mara, Tanzania
Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Neema Ibamba akizungumza wakati wa utambulisho wa mradi wa Anaweza unatarajiwa kutekelezwa na Shirika lilisilokuwa la kiserikali la Youth Empowering Initiative (YEI) katika wilaya za Musoma na Bunda mkoani Mara.
Milioni 30 za Kitanzania zinatarajiwa kutumika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuwajengea uwezo wanawake vijana katika halmashauri mbili za Mkoa wa Mara.
Katika mradi huo wa mwaka mmoja ambao umepewa jina la ‘Anaweza’, utawanufaisha wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35 katika kata sita ambao utatekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la Youth Empowering Initiative (YEI).
Akitambulisha mradi huo mjini Musoma Agosti 9, 2023, Ofisa miradi wa shirika hilo, Pulietha Massao amesema hadi kukamilika kwa mradi huo walengwa watakuwa na uwezo wa kupambana na mila kandamizi zinazosababisha kuwapo kwa ukatili wa kijinsia.
“Tumebaini kuwa wapo watu wengine wanaofanyiwa vitendo hivi lakini kutokana na kutokuwa na uelewa au kutokuona umuhimu wa kutoa taarifa wanaamua kukaa kimya hali hii inachangia kuendelea vitendo hivi na kukosesha takwimu sahihi,” amesema
Amesema walengwa hao pamoja na kupewa elimu namna ya kuepuka vitendo vya ukatili, pia watapewa elimu ya ujasiriamali ili wawe na uwezo wa kuanzisha miradi midogo midogo itakayowawezesha kuwa na vyanzo vya uhakika wa kipato kwani ukosefu wa vyanzo hivyo ni mojawapo ya kichocheo cha vitendo vya ukatili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Theresia Buhatwa amesema mradi huo unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii kuhusu vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.
“Tunatarajia mradi huu uwe sehemu ya kuleta mabadiliko katika jamii kwa kuweka mazingira salama na rafiki kwa vizazi vya sasa na vijavyo, na ni matamanio yetu kuwa tuwe na mradi kama huu katika wilaya za Tarime na Serengeti ila kuokana na ufinyu wa bajeti tumeamua kuanza na hizi wilaya mbili kwanza,” amesema
Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Neema Ibamba amesema uwepo wa mashirika yanayotetea haki za binadamu hususani watoto na wanawake katika mkoa huo kumesaidia kuleta mabadiliko chanya juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Vitendo bado vipo lakini kuna mabadiliko makubwa, kwasasa sina takwimu lakini hali halisi inajionyesha kuwa watu wamebadilika,” amesema
Wanaharakati wa mapambano ya udhalishaji wa kinjinsia