Na Charles Wasonga, Nairobi
HISIA mseto zimeibuliwa kuhusu iwapo hatua ya Rais William Ruto kutumia nguvu za dola kunyamazisha mahasidi wake wa kisiasa itamfaa au kumgharimu kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Baadhi wa wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanaonya kwamba mbinu hii iliyotumiwa na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta na Hayati Daniel Moi, itayeyusha ushawishi wake katika maeneo mbalimbali nchini.
Kulingana na Bw Herman Manyora, ni mapema zaidi kwa Rais Ruto kuanza kutumia maafisa wa polisi kama silaha za kumsaidia kuendesha vita vyake vya kisiasa dhidi ya upinzani.
“Dkt Ruto akumbuke kuwa ni juzi tu ambapo mbinu ilipotumiwa dhidi yake yake na wandani wake ilimgharimu mtangulizi wake, Bw Kenyatta. Hizi mbinu za kimla zimepitwa na wakati,” akasema Bw Manyora ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu uliopita Dkt Ruto alisema chini ya utawala wake polisi hawataingilia kisiasa katika utendakazi.
“Hatutarudia makosa ya hawa tunaoshindana nao ambao wamegeuza polisi kuwa wanasiasa. Polisi wetu watatumiwa kuwinda wahalifu sugu na wakora wengine wala sio wanasiasa,” akasema mnamo Juni 30, 2022 alipoongoza hafla ya uzinduzi wa manifesto ya Kenya Kwanza katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Nairobi.
Kwa upande wake Philip Cheburet anasema maafisa wa polisi wanafanyakazi kazi yao ya kulinda mali na maisha kwa kuwakamata wanasiasa wanaotumia maandamano kama kisingizio cha kuchochea uhalifu.
“Kwa mfano, muungano wa sekta kibinafsi (Kepsa) juzi ulikadiria kuwa Kenya imekuwa ikipoteza Sh3 bilioni kila siku wakati wa maandamano. Kipengele cha 37 cha Katiba maandamano ya amani wala sio uharibifu wa mali,” anasema tangu Machi mwaka huu, upinzani ulipoanza kuitisha maandamano dhidi ya serikali wabunge kadha wa upinzani wamekamatwa kwa madai ya kupanga kushiriki maandamano haramu.
Wiki hii, wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki), Ken Chonga (Kilifi Kusini), Anthony Oluoch (Mathare) na Spika wa Bunge la Kaunti ya Kilifi Teddy Mwambire walikamatwa kwa madai walipanga kuzuia fujo na uharibifu wa mali wakati wa maandamano.
Wengine waliokamatwa ni mlinzi wa Bw Odinga Maurice Ogeta na msemaji wake Dennis Onyango na watu waliodaiwa kuwa maafisa wa polisi waliovalia mavazi ya kiraia.
Aidha, wakereketwa wengine wa Azimio kutoka sehemu mbalimbali za nchini, akiwemo Calvins Okoth, almaarufu Gaucho, wamekamatwa kwa njia ya kutatanisha.
Kando hayo serikali imewaondoa walinzi wa Bw Odinga, Kalonzo Musyoka, zaidi na wabunge 50 wa muungano huo, katika kile kinachoonekana kama mbinu ya kuwatisha ili wapunguze kampeni za kuikosoa serikali.
Wengine waliopokonywa ulinzi ni magavana kutoka eneo la Nyanza ambao ni pamoja na Simba Arati (Kisii), James Orengo (Siaya), Ochilo Ayack (Migori), Profesa Peter Anyang’ Nyong’o (Kisumu) na Gladys Wanga (Homa Bay).
Hii ni mara ya tatu Bw Odinga na Musyoka, kupokonywa walinzi, chini ya utawala wa Dkt Ruto kutokana na kile kinachosawiriwa kama sababu za kisiasa.
Lakini kisheria, wawili hao wanayo haki ya kupewa ulinzi na serikali kwa misingi ya afisi walizozishilia awali.
Bw Odinga ni Waziri Mkuu wa pili wa taifa la Kenya ilhali Bw Musyoka ni Makamu wa 10 nchini Kenya na alihudumu katika muhula wa pili wa Hayati Mwai Kibaki.
Lakini kile ambacho kimewaacha wengi vinywa wazi ni hatua ya kupokonywa kwa walinzi wa Mamake Bw Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta kutokana sababu hizo hizo za kisiasa.
Hatua hiyo ilichukuliwa, pasina nyanya huyo mwenye umri wa miaka 90 kujulishwa, mnamo Jumatatu wiki hii, siku kadha baada ya Rais Ruto na wandani wake kudai kuwa Bw Kenyatta ndio anafadhili maandamano ya Azimio.
Mama Ngina amekuwa akipata ulinzi wa serikali katika makazi yake ya Muthaiga, Nairobi na Ichaweri, Gatundu Kusini, kaunti ya Kiambu, tangu mumewe Rais wa Kwanza Hayati Mzee Jomo Kenyatta alipofariki mnamo 1978.
Baada ya kuondolewa kwa walinzi hao wa serikali imemlazimu Mama Ngina kukodi huduma za walinzi wa kibinafsi.
William Ruto.