Na Waashirika Wetu
MTINDO unaotumiwa na vikosi vya usalama kuwakamata wanasiasa wanaoegemea mlengo wa Azimio la Umoja na kukabiliana na watu wanaojitokeza kushiriki maandamano, inazua maswali kuhusu iwapo ni polisi au ni magenge ya kukodishwa yataleta amani ama machafuko.
Baadhi ya wanaowakabili waandamanaji hawavai sare za polisi, hawatumii magari rasmi ya polisi mbali na kutumia nguvu kupita kiasi ikiwemo dhidi ya watoto, kuwatoa watu ndani ya nyumba zao na kuwapiga kiholela.
Wengine wamekuwa wakiwarushia mawe waandamanaji na hata kuwavamia watu wasioandamana. Viongozi wa Upinzani wamedai kuwa kuna magenge yaliyolipwa na wanasiasa kushambulia wafuasi wao yakilindwa na polisi.
Mbinu zinazotumiwa kuwakamata wanasiasa hao na wafuasi wao zimezua maswali, huku ikiripotiwa kuwa waathiriwa wanatekwa nyara kabla ya kuzuiliwa kwa zaidi ya saa 24 kinyume cha sheria.
Kwa kawaida, polisi wanafaa kufuata taratibu zinazoheshimu haki za mshukiwa zinazojumuisha kumweleza makosa yake na kumruhusu kuwasiliana na familia na mawakili wake.
Baadhi ya wanasiasa na watu waliokamatwa katika hali tatanishi ni wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki), aliyekuwa kiongozi wa kundi la Mungiki, Maina Njenga, mlinzi wa Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga -Maurice Ogetta, mwanablogu wa mrengo wa Azimio Pauline Njoroge na mbunge Anthony Oluoch (Mathare).
Hadi jana, ni Babu Owino pekee ambaye alikuwa amefikishwa kortini miongoni mwa waliotajwa hapo juu.
Bw Ogeta aliachiliwa huru baada ya kuzuiliwa kwa saa 72 bila kufikishwa kortini inavyohitaji sheria.
Tukio jingine ambalo limezua maswali ni uvamizi uliotekelezwa na katika makazi ya mwanawe Rais Mstaafu Uhuru, Jomo Kenyatta, Ijumaa usiku, katika mtaa wa Karen, jijini Nairobi na maafisa wa polisi bila kibali rasmi.
Ingawa Serikali ilikiri polisi walifanya uvamizi huo, sheria inahitaji polisi kupata kibali cha mahakama au kuita mtu kwanza kujiwasilisha kwao.
Kulingana na wakili wake, Bw Ndegwa Njiru, Bw Owino alizuiliwa kwa muda na baadaye kusafirishwa hadi katika Kituo cha Polisi cha Wang’uru, kilicho katika Kaunti ya Kirinyaga, nyakati za usiku.
“Bw Owino alikamatwa na watu waliojitambulisha kama maafisa wa DCI na kusafirishwa usiku hadi katika Kituo cha Polisi cha Wang’uru. Swali ni je, ni kwa sababu gani watu hao walimkamata usiku bila kumwambia makosa yake.
“Pili, kwa kawaida, polisi huwa na kibali cha kumkamata mtu. Tatu, mbona walimzuiliwa zaidi ya saa 24? Haya ni baadhi ya maswali tunayoibua kuhusu uhalali wa kamata kamata zinazoendelezwa dhidi ya viongozi,” akasema Bw Njiru.
Bw Maina Njenga anadaiwa kukamatwa Jumatano usiku na watu wasiojulikana katika eneo la Olosurutia, Kaunti ya Kajiado.
Mnamo Jumamosi, mawakili na jamaa zake walisema kuwa licha ya sheria kuwahitaji polisi kumfikisha mahakamani saa 24 baada ya kukamatwa kwake, hajafikishwa katika mahakama yoyote.
Inadaiwa Maina alikamatwa pamoja na ndugu zake wawili na msaidizi wake wa kibinafsi, aliyetambuliwa kama Ole Lekishe.
“Bw Maina alikamatwa na polisi akiwa amemtembelea babake anayeugua. Alikamatwa na polisi waliokuwa na sare rasmi na wengine ambao hawakuwa nazo. Hadi sasa, hatujui mahali walipompeleka kama familia na marafiki zake. Tumeenda karibu vituo vyote vya polisi ila hatujapata jibu lolote. Swali letu kwa serikali ni: yuko wapi Maina Njenga?” akauliza mmoja wa jamaa yake, aliyejitambulisha kama Bw Murungaru.
Bw Ogeta alieleza kwa kina madhila aliyopitia baada kutekwa nyara.
Alisema alifungiwa kwenye chumba kidogo tu na kufungwa macho ili asione chochote kilichokuwa kikiendelea hadi alipoachiliwa. Alisema hakufahamu makosa yake.
“Tangu niingie huko, niliwekwa katika hali ambapo nisingeweza kuzungumza na yeyote. Sikujua kilichokuwa kikiendelea kwa sababu sikuwa na simu na chumba chenyewe hakikuwa na runinga. Kile nilichoweza kufanya ni kuangalia dari (paa) na ukuta. Sidhani kile kilikuwa kituo cha polisi,” akasema Bw Ogeta, muda mfupi baada ya kuachiliwa.
Alitupwa barabarani saa saba usiku katika eneo la Ruai, Nairobi wahalifu wanavyofanyia watu.
Kulingana na Mkuu wa Mawasiliano katika chama cha ODM, Bw Philip Etale, Bw Oluoch alikamatwa Alhamisi usiku na watu waliodai kuwa polisi katika kituo kimoja cha mafuta. Alikuwa akiliweka gari lake mafuta.
“Alikamatwa na kuwekwa kwenye gari lenye nambari za usajili za Tanzania,” akasema Bw Etale.
Hapo jana, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi aliitaka serikali kuyaondoa makundi yote yenye silaha yanayohudumu katika Idara ya Polisi.
“Kama viongozi, tunashurutisha serikali kuyaondoa makundi yote yaliyojihami yanayowaua watu wetu katika eneo la Nyanza,” akasema Bw Opiyo, kwenye taarifa aliyotoa jana kwa niaba ya wabunge kutoka ukanda wa Nyanza.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu pia yamekuwa yakieleza kuhofishwa na mbinu ambazo polisi wamekuwa wakitumia kuwakamata na kuwakabili waandamanaji.
Maandamoano yanayoendelea nchini Kenya.