Na Mwandishi Wetu
Bodi ya Wakandarasi Nchini (CRB), imesimamisha ujenzi wa mradi wa ghorofa mbili unaojengwa maeneo ya Mbezi kwa Yusufu jijini Dar es Salaam.
Meneja wa CRB, kanda ya Mashariki Dar es Salaam, Mhandisi Ally Mwita alisema tayari wamekwisha simimisha ujenzi wa mradi huo na mkandarasi aliyekuwa anasimamia mradi huo amepigwa faini ya Tsh1,500,000.
Alisema kuwa usajili wa mradi wa ujenzi unafanyika kwenye mfumo mtandaoni, na wakandarasi wote wanapatiwa jina la mtumiaji na neno la siri hivyo ni vigumu kwa mtu asiyehusika kuweza kusajili mradi.
Aliongeza kuwa kampuni iliyokuwa inasimamia mradi huo ilikubali kulipa faini baada ya kubaini kuwa walikuwa wanaendesha mradi chini ya ukomo wao wa kuendesha miradi kulingana na daraja la kampuni hiyo ambayo ni daraja la tano na mradi huo ni zaidi ya milioni 500.
“Tulisajili mradi kulingana na nyaraka zilizowasilishwa kwetu..baada ya kwenda kwenye ukaguzi tulibaini kuwa mradi ni mkubwa na kampuni hiyo imepigwa faini,” alisema Mwita
Akaongeza kuwa haiwezekani kuwa mtu asiyehusika akasajili mradi, kwani kila tunaposajili mradi tunatuma ujumbe kwa mhusika wa kampuni ili kama hana taarifa na mradi huo aweze kutoa taarifa kusitisha zoezi la usajili.
Alisema kuwa kampuni hiyo kama walikuwa hawana taarifa na mradi huo kwa nini waliamua kulipa faini baada ya kutozwa faini na bodi kwa kuendesha mradi mkubwa kinyume na uwezo wake .
Mwita alikuwa akitoa ufafanuzi kuhusu mradi huo ambao unadaiwa kuwa kigogo mmoja anayefanya kazi Chuo cha Kodi kilichopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, ambaye pia alikuwa mgombea wa nafasi ya NEC kupitia wazazi Ubungo, Joseph Masatu Chikongoye , anadaiwa kukiuka sheria za ujenzi na ukwepaji wa kodi.
Taarifa za uchunguzi zinadai kigogo huyo kwa kushirikiana na injinia wake walikiuka kwa kushindwa kufuata taratibu za ujenzi.
Inadaiwa kuwa mradi wa jengo la biashara umejengwa na kusimamiwa na injinia anayefahamika kwa jina la John ambaye hatambuliki kwenye Bodi ya Wahandisi (ERB), na sio mfanyakazi wa kampuni ya ujenzi.
Pia, inadaiwa kuwa malipo ya ununuzi wa vifaa na malipo ya kazi katika mradi huo yamekuwa yakilipwa mkononi bila kupitia akaunti za kampuni zinazofanya ujenzi ili kuwezesha kulipa kodi za serikali,
Inadaiwa kuwa mradi wa ujenzi huo una thamani ya milioni 542, na bango la mradi (sign board) iliyoko kwenye mradi inaonesha kuwa mkandarasi anayesimamia mradi huo ni kampuni ya ZIONANE CONTRACTORS & GENERAL SUPPLIES COMPANY LIMITED ambayo ni daraja la 5, uwezo wake wa ukomo wa kufanya miradi ya ujenzi (class limit) ni milioni 300.
Kwa mujibu wa taarifa inadaiwa kuwa mkurugenzi wa kampuni hiyo ya JAJI CONSULT CO. LTD ambayo bw Chingoye anahusishwa kwa kutumia nafasi yake ya kazi na uwezo wa kifedha, waliweza kununua bango la mradi wa ujenzi huo na kusajili mradi bila kufuata taratibu za ujenzi kwa kushirikiana na maafisa wa Bodi ya Wakandarasi (CRB) wasio waaminifu na kufanikiwa kukwepa kodi na kuendesha mradi wa ujenzi wa mamilioni ya shilingi bila kutumia kampuni za ujenzi.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Morningstar POST, kigogo huyo, anadaiwa kujenga mradi wa ujenzi wa jengo la biashara la ghorofa mbili, maeneo ya Mbezi Kwa Yusufu la zaidi ya thamani ya milioni 500 bila kutumia wakandarasi.
Kwa mujibu wa bango la ujenzi lililowekwa kwenye mradi huyo, Mkandarasi aliyeorodheshwa hana mkataba na kigogo huyo na kampuni yake haina uwezo wa kujenga jengo lenye thamani ya milioni 500 licha ya kuwa limewekwa katika mradi huo kama ndio mkandarasi anayesimamia ujenzi.
Hata hivyo, bango la ujenzi lililopo kwenye mradi huu inadaiwa limeibwa na makampuni yaliorodheshwa kwenye bango hilo hawana mkataba na kigogo huyo.
Hata hivyo tunaendelea kuwatafuta viongozi Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kuzungumzia mradi huo kutokana na ukwepaji wa kodi.
0713685823
Mradi wa ujenzi wa jengo la biashara la ghorofa mbili lililoko Mbezi kwa Yusufu Magari Saba uliosimamishwa na CRB