Mto Luhanya ulioko mtaa wa Bonyokwa Kata ya Bonyokwa jijini Dar es Salaam, umegeuzwa dampo la kutupwa takataka hatari za mahosptalini.
Kwa mujibu wa wakazi wa mtaa wa Bonyokwa maeneo ya mto huo ambao chanzo chake ni mto Msimbazi, wamesema kuwa taka nyingi za hosptali zimekuwa zikitupwa katika mto
huo na watu wasiojulikana.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Bonyokwa Shabani Maliyatabu alipoulizwa na Morningstar Post kuhusiana na uchafuzi wa mazingira katika mto huo unaotenganisha manispaa ya Ubungo na Ilala unaofanywa na watu wenye hosptali katika maeneo hayo alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi.
Aliongeza kuwa wananchi walimpingia simu kumpa malalamiko hayo ya kutupwa kwa taka za mahosptali katika mto huo na kuwataka kwenda kwa mjumbe wake wa afya na mazingira wa eneo husika ili kushughulikia suala hilo.
“Nikweli hata mimi nilipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu suala la kuwepo
kwa taka za hosptali kwenye mtoa huo..alisema Maliyatabu.
Alisema kuwa baada ya kufuatilia aliona taka taka hizo mtoni lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa zililetwa na maji kwenye mto huo.
Alisema kuwa hawezi kuthibitisha kuwa taka hizo zimetupwa na watu wa hosptali ya Harmony kwa kuwa hajawabaini kufanya hivyo.
Bw Malitabu alisema kuwa baada ya kupokea taarifa hizo ameweka mtego kuwabaini wanaofanya hivyo kutupa taka za hosptali kwenye mto huo kupitia kamati yake ya
afya na mazingira.
Morningstar POST ilifika kwenye mto huo na kuzungumza na baadhi ya wakazi wa mtaa huo ambao hawakupenda kutajwa majina yao walidai kuwa taka hizo zimekuwa
zikitupwa na hosptali iliyoko karibu na mto huo.
Walisema kuwa wakati mvua inaponyesha kumekuwa na taka nyingi za mahosptali katika mto huo ambazo ni hatari kwa afya za watu.
Akizungumza na Morningstar Post, Afisa Utawala wa hosptali ya Harmony Memorial Polyclinic ambayo iko mita chache kutoka kwenye mto huo, Bi, Rose Kabika, alikanusha taarifa za hosptali yao kuhusika kutupa taka hizo.
Alisema kuwa hosptali yao ina kifaa cha kuteketeza taka za hosptali hivyo hawana sababu ya kutupa taka kwenye mto huo.
Aliongeza kuwa inawezekana kuwa taka hizo zimetoka mbali kwakuwa maeneo hayo kuna idadi kubwa ya hosptali ambazo hazina vifaa vya kuteketeza taka za hosptali.
Hata hivyo Morniningstar Post ilishuhudia kifaa cha kuteketeza taka cha hosptali hiyo kikiwa kimefurika taka na mlango wa kifaa hicho ukiwa umeharibika na taka nyingine zikiwa zimewekwa pembeni ya kifaa hicho.
Timu ya uchunguzi ya Morningstar POST inaendelea kufuatilia chanzo cha uchafuzi wa mto huo
.
