Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini (TMDA), imetoa adhabu na onyo kali kwa mmiliki wa duka la dawa la Shamshudin lililoko jijini Dar es Salaam kwa kuuza madawa yasiyosajiliwa hapa nchini.

Akizungumza na Morningstar POST ofisini kwake, Meneja wa TMDA Kanda ya Mashariki, Bw. Adonis Bitegeko alisema duka hilo lililoko maeneo ya katikati ya jiji mtaa wa Mshihiri na Sunil, limetozwa faini ya shilingi 3,300,000 kwa kukutwa na dawa ambazo hazijasajiliwa na mamlaka hiyo na tayari wameshalipa faini hiyo.

Pia, Bitegeko amesema kuwa TMDA imetaifisha madawa yote yaliokamatwa katika duka hilo na yanafanyiwa utaratibu wa kuteketezwa.

“Ni kweli tulifanya ukaguzi na kugundua madawa ambayo hayajasajiliwa kwenye duka la Shamshudin…madawa ya aina ya tiba asili baada ya kubaini tulikamata na kumpiga faini na kumpa barua ya onyo kali”, alisema Bitegeko.

Akaongeza kuwa mbali na adhabu ya faini, lakini pia kitendo cha kutaifisha madawa hayo kwa lengo la kuyateketeza ni adhabu na amepewa onyo kwa barua kutokuendelea kuuza dawa zisizosajiliwa.

Bw. Bitegeko alisema kuwa hatua itakayofuata baada ya kupigwa faini watakuwa wakimfanyia ukaguzi mara kwa mara na iwapo itabainika kufanya udanganyifu wa aina yoyote atafungiwa kufanya biashara hiyo.

“Hatua ya kwanza huwa tunatoa adhabu na kumpa onyo kali, ili itakapojitokeza tena hatakuwa na utetezi wa aina yoyote ni kumfungia tu”, alisema.

Aidha, Bw Bitegeko alichukua fursa hiyo kuwaasa wananchi na wafanyabiashara wote wa madawa kuhakikisha wanafuata sheria, kwani mamlaka yake inazingatia sheria, usalama, ubora, ufanisi na kuhakisha nidhamu bila kupindisha sheria.

Bw. Bitegeko alitoa ufafanuzi huo baada ya (TMDA), kufanikiwa kukamata madawa mbalimbali yasiyosajiliwa na kuuzwa kwenye duka hilo na Morningstar POST kuandika taarifa hiyo.

Morningstar POST ilishuhudia zoezi la ukaguzi na ukamataji wa madawa hayo kwenye duka hilo maeneo ya katikati ya jiji mtaa wa Mshihiri na Sunil, siku chache zilizopita.

Meneja wa TMDA Kanda ya Mashariki, Bw. Adonis Bitegeko

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *