Na Mwandishi Wetu

Maafisa wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Nchini (TMDA), wamefanikiwa kukamata madawa mbalimbali yasiyosajiliwa na kuruhusiwa kuuzwa kwenye duka la dawa la Shamshudin lililoko jijini Dar es Salaam.

Morningstar POST ilishuhudia zoezi la ukaguzi na ukamataji wa madawa hayo kwenye duka hilo maeneo ya katikati ya jiji mtaa wa Mshihiri na Sunil, siku chache zilizopita.

Maafisa wa TMDA walifika katika duka hilo baada ya kupata taarifa kuwa duka hilo linajihusisha na kuuza dawa hatari ambazo hazijasajiliwa hapa nchini, wakiwa na gari la serikali namba STL 6358 na kufanya upekuzi kwenye duka hilo.

Zoezi la upekuzi na ukamataji wa madawa hayo ulianza majira ya saa tisa alasiri na kumalizika saa mbili usiku ambapo maafisa hawa waligundua madawa mbalimbali ya binadamu yasiosajiliwa na kuruhusiwa kuuzwa dukani hapo.

Maafisa hao walionekana kutoka ndani ya duka hilo majira ya saa mbili usiku na boksi kubwa la madawa yaliokamatwa ambayo hayaruhusiwi kuuzwa kwenye duka hilo.

Hata hivyo, walipoulizwa na mwandishi wa habari hizi walishindwa kutoa maelezo zaidi kwa madai kuwa wao sio wasemaji wa TMDA.

Chanzo cha habari kutoka ndani ya duka hilo ambaye alishuhudia zoezi hilo ndani ya duka hilo na kutopenda kutajwa jina lake, alisema TMDA, wamefanikiwa kukamata madawa aina mbalimbali (kama yanavyoonekana kwenye picha ya stori hii).

“Wamekagua madawa na kukuta madawa mengi sana yasiotakiwa na mengine yasiosajiliwa….pia na ile dawa aina ya Himplasia nayo ilikutwa,” alisema.

Akaongeza kuwa wakati wa zoezi hilo muuza duka hilo alipotakiwa kufungua droo mojawapo kwenye meza za duka hilo alikataa hadi maafisa wa TMDA walipotishia kuita polisi ndipo alifungua na kukuta dawa aina ya Himplasia ambayo tovuti hii iliripoti kuwa inauzwa kwenye duka hilo.

Alisema kuwa baada ya TMDA kukamata madawa hayo waliondoka nayo ofisini na kumtaka muuza duka kufika ofisini kwao kwa ajili ya kulipa faini na taratibu zingine za kiofisi.

Duka hilo maarufu linalouza dawa mbalimbali za binadam kwa jumla na rejareja, limebainika kuuza baadhi ya dawa ambazo hazijasajiliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Morningstar POST, iliandika habari kuhusu duka hilo kuuza dawa aina ya Himplasia inayosaidia matatizo ya uzazi ikiwemo nguvu za kiume.

Baada ya kuandika habari za uuzaji wa dawa hizo kwenye duka hilo baada ya kununua dawa hizo zinazotengenezwa na kampuni ya Himalaya ya nchini India, TMDA walifika na kubaini madawa mengine zaidi yasiotakiwa.

Juhudi za kuwapata viongozi wa TMDA kuzungumzia zoezi hilo hazikuweza kufanikiwa mara moja isipokuwa tunaendelea kuwatafuta kwa ajili ya kujua taarifa zaidi zilizochukuliwa dhidi ya duka hilo ambalo linaendelea kuuza dawa.

Madawa aina mbalimbali yaliokamatwa na TMDA kwenye duka la dawa la Shamshudin Dar es Salaam hivi karibuni

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *