Na Mwandishi Wetu

Duka la dawa la Shamshudin lililoko jijini Dar es Salaam, maeneo ya katikati ya jiji mtaa wa Mshihiri na Sunil, linajihusisha na kuuza dawa hatari ambazo hazijasajiliwa hapa nchini.

Duka hilo maarufu linalouza dawa mbalimbali za binadam kwa jumla na rejareja, limebainika kuuza baadhi ya dawa ambazo hazijasajiliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Morningstar POST, ulifanywa kwa nyakati tofauti, umebaini kuwa duka hilo linauza dawa aina ya Himplasia inayosaidia matatizo ya uzazi ikiwemo nguvu za kiume.

Morningstar POST, imefanikiwa kubaini uuzaji wa dawa hizo kwenye duka hilo baada ya kununua dawa hizo zinazotengenezwa na kampuni ya Himalaya ya nchini India.

Mwandishi wa habari hizi alinunua dawa hizo kutoka kwenye duka hilo mara kadhaa kwa bei ya sh18,000 bila kupewa lisiiti ya aina yoyote na kuulizwa maelezo ya daktari.

Licha ya dawa hiyo kutosajiliwa na TMDA, boksi la dawa hiyo limeandikwa maelezo kuwa dawa hiyo inatakiwa kuuzwa nchini India na Napal tu, lakini duka hilo limekuwa likiuza hapa nchini bila kuisajili.

Mmoja wa wateja walionunua dawa hiyo pia kutoka kwenye duka hilo, ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alisema kuwa alinunua dawa hiyo na baada ya kutumia ilimletea madhara ya kuhisi kizunguzungu.

Aliongeza kuwa baada ya kujihisi kizunguzungu alifika Kituo cha Afya Mnazi Mmoja ambako daktari alionesha kumshangaa kutokuifahamu dawa hiyo aliyotumia.

“Baada ya kueleza madaktari walinishangaa kwani hawaijui hiyo dawa…..niliwaambia kuwa nilipewa dawa hiyo kutibu tatizo la tezi dume, walinishangaa sana,” alisema.

Alisema kuwa aliuziwa dawa hiyo zaidi ya mara moja na kila anapokuwa ananunua haulizwi cheti cha daktari na hapewi lisiti, lakini kilichomshtua zaidi ni katazo lililoko kwenye boksi ya dawa hizo kuwa zinatakiwa kuuzwa nchini India na Napal tu.

Alipotakiwa kujibu tuhuma hizo za kuuza dawa ambayo haijasajiliwa, muuzaji wa duka hilo ambaye alikataa kujitambulisha jina lake alisema kuwa msemaji wa duka hilo ambaye ni mfamasia amesafiri nje ya nchi atarejea baada ya siku mbili.

Muuza duka huyo ambaye namba yake ya simu alioitoa kwa mwandishi wa habari hizi, usajili wake unasomeka kwa jina la Mubin Gothey baada ya siku mbili alipoulizwa tena alijibu kuwa msemaji ajarudi na kama tunataka kuandika habari hizo ziandikwe.

“|Kama unataka kuandika andikeni, nyinyi si ndio mliokuja juzi hapa….bado hajarudi anarudi leo, akitokea ntawataarifu,” alisema.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *