Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amewataka watumishi wa Wizara ya Ujenzi na Taasisi zake kuongeza ubunifu, kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha huduma kwa wananchi zinatolewa kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.

Eng. Kasekenya ameyasema hayo mkoani Dodoma, wakati akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu katika kikao kati ya Kamati hiyo na Viongozi wa Wizara ya Ujenzi pamoja na Taasisi zake.

Amesema wananchi hufarijika wanapopata huduma bora kutoka Serikalini na katika Taasisi zake kwa wakati, akisisitiza kuwa wananchi ndio wadau wakubwa wa Serikali na wanapohudumiwa vizuri hujenga imani kwa Serikali na kupata ari ya kushiriki katika shughuli za maendeleo.

“Mdau mkubwa wa Serikali ni wananchi, hivyo wakihudumiwa vizuri wanapata ari ya kuiamini Serikali na kufanya shughuli zao za maendeleo kwa furaha,” amesisitiza Eng. Kasekenya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso, ameishukuru Wizara ya Ujenzi kwa ushirikiano unaotolewa kwa Kamati hiyo, akisema ushirikiano huo umechangia katika kubaini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za miundombinu nchini.

Mhe. Kakoso ameitaka Wizara kuhakikisha inaendelea kuziwezesha Taasisi zake, zikiwemo TANROADS, TBA na TEMESA, ili ziweze kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa Serikali na wananchi kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Kakoso amesema kuwa takribani asilimia 90 ya mizigo yote nchini husafirishwa kwa njia ya barabara, huku asilimia 80 ya abiria wakitumia usafiri wa barabara. Kwa msingi huo, amesisitiza umuhimu wa kuwa na mtandao bora na salama wa barabara katika kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo ya wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *