Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kuwa ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike (km 70) ni muhimu katika kuchochea shughuli za kiuchumi na kufungua fursa za biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, pamoja na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na nchi jirani.

Ulega ameyasema hayo mkoani Katavi wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike, ambapo amesema Serikali itaendelea kuhakikisha inatenga na kutoa fedha kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo kukamilika kwa mujibu wa viwango na muda uliokusudiwa.

Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo, kuongeza fursa za biashara na kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko, hivyo kuchochea maendeleo ya wananchi wa Katavi na mikoa jirani.

Aidha, Ulega amesema Serikali tayari imelipa Shilingi bilioni nne kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Mpanda–Kigoma, huku akimtaka Mkandarasi kuhakikisha anamalizia kwa haraka ujenzi wa Daraja la Mnyamasi ili kurahisisha matumizi ya barabara hiyo na kuzuia changamoto za mawasiliano wakati wa msimu wa mvua.

Waziri huyo amesisitiza kuwa wasimamizi wa miradi wanapaswa kuhakikisha maeneo yote yanayokatisha mawasiliano wakati wa mvua yanapatiwa ufumbuzi wa kudumu, huku akielekeza kazi zifanyike kwa kasi bila kuathiri ubora wa miundombinu inayojengwa.

Awali, akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi, Eng. Martin Mwakabende, amesema utekelezaji wa ujenzi wa kipande cha kwanza cha barabara hiyo umegawanywa katika sehemu tatu, huku gharama ya ujenzi ikiwa ni Shilingi bilioni 88.72.

Ujenzi wa Barabara ya Kibaoni–Sitalike ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuimarisha mtandao wa barabara nchini, kurahisisha usafirishaji na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi katika maeneo yanayounganishwa na barabara hiy

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *