Na OWM-TAMISEMI, Iringa
Bingwa mtetezi wa mpira wa netiboli wa UMITASHUMTA 2025, Mwanza, imeendelea kuonyesha jeuri na dhamira ya kulitetea kombe lake baada ya kutinga fainali ya mashindano ya UMITASHUMTA 2026 kufuatia ushindi mkubwa wa magoli 69-25 dhidi ya Songwe katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Juni 15, 2026 mkoani Iringa.
Mwanza ilionyesha ubora mkubwa kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo huo, huku ikitawala maeneo yote ya uwanja na kutumia vyema nafasi zilizojitokeza kufunga magoli mengi yaliyoiwezesha kupata ushindi huo mnono na kuendelea kubaki kwenye mbio za kutwaa ubingwa kwa mara nyingine mfululizo.
Katika mchezo mwingine wa nusu fainali, Simiyu nayo ilithibitisha ubora wake baada ya kuichapa Iringa kwa magoli 60-31 na kufanikiwa kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali ya mashindano hayo. Ushindi huo umeifanya Simiyu kuwa mpinzani wa Mwanza katika pambano la kuwania taji la netiboli UMITASHUMTA 2026.
Matokeo hayo yamezikatisha ndoto za Iringa na Songwe za kutwaa ubingwa, hata hivyo timu hizo zitapata nafasi ya kuwania medali ya shaba katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu utakaochezwa kesho asubuhi kabla ya pambano la fainali.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano, Iringa itamenyana na Songwe katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu, huku macho na masikio ya wadau wengi wa michezo yakielekezwa kwenye mchezo wa fainali kati ya Mwanza na Simiyu ambao unatarajiwa kuwa wa ushindani mkubwa kutokana na kiwango kizuri kilichoonyeshwa na timu hizo katika hatua mbalimbali za mashindano.
Mwanza sasa itashuka dimbani ikiwa na lengo la kutetea ubingwa wake na kurejesha tena kombe nyumbani, wakati Simiyu ikisaka kuandika historia mpya kwa kutwaa taji la UMITASHUMTA 2026.