Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji mkoani Singida kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Akizungumza leo wakati wa ziara ya Waziri Mkuu mkoani Singida, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya miundombinu ili kuimarisha mawasiliano kati ya Mkoa wa Singida na mikoa jirani.

Alisema miongoni mwa hatua zinazotekelezwa ni pamoja na kuboresha barabara za mkoa huo, kupanua barabara katika eneo la Mlima Sekenke na kujenga madaraja mapya yatakayorahisisha usafiri wa wananchi pamoja na usafirishaji wa bidhaa.

Mhandisi Kasekenya alibainisha kuwa Serikali tayari imekamilisha ujenzi wa madaraja mawili muhimu katika Jimbo la Iramba, ambayo ni Daraja la Mwajuma na Daraja la Kokilangi. Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kumeondoa changamoto za usafiri zilizokuwa zikiwakabili wananchi, hasa wakati wa msimu wa mvua.

Aidha, alisema maboresho yanayoendelea katika Sekta ya Ujenzi yanalenga kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara, kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa na huduma, na kufungua fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na maeneo ya jirani.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba yuko mkoani Singida kwa ziara ya kikazi inayolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kufanya mikutano ya hadhara, kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kutoa maelekezo yatakayosaidia kuharakisha maendeleo katika mkoa huo.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *