Na Cletus Sanga, WAF – Morogoro

Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia ufadhili wa Pandemic Fund imeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya nchini.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa, Dkt. Erasto Sylvanus, wakati wa kufunga mafunzo kwa ajili ya kujenga uwezo wa Timu ya Kitaifa itakayotoa matibabu (EMT 10 Steps and EMTCC) kipindi cha dharura na maafa nchini, yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Dkt. Sylvanus amesema ni muhimu kwa wataalamu waliopata mafunzo hayo kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuimarisha taasisi walizotoka, huku wakihakikisha wanaendelea kuzingatia viwango, miongozo na taratibu za kitaifa na kimataifa katika kupanga, kutekeleza na kutoa mwitikio wa huduma za dharura.

Amesisitiza kuwa wataalamu hao wanapaswa kuwa tayari wakati wote kuitumikia nchi pale watakapohitajika, ndani na nje ya nchi, kwa kuzingatia uzalendo, nidhamu, weledi na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kama timu.

Aidha, amewataka kutambua kuwa wanapokuwa katika majukumu ya dharura wanaiwakilisha nchi pamoja na Wizara ya Afya hivyo wanapaswa kulinda heshima na taswira yake.

Ameongeza kuwa uanzishwaji na uhuishaji wa kanzidata ya wataalamu wa Timu za Dharura za Afya utasaidia katika kupanga na kuratibu rasilimali watu kwa ufanisi wakati wa matukio ya dharura.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Bi. Janeth Masuma, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha mifumo ya utayari na mwitikio wa dharura za afya nchini kupitia uwekezaji katika kujenga uwezo wa wataalamu.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha nchi inakuwa na uwezo wa kukabiliana kwa haraka na matukio mbalimbali ya dharura za afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *