NA MWANDISHI WETU
KUMEBAINIKA mkakati wa kumchafua Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya Benjamin Kuzaga, kwa kumuhusisha na tuhuma mbalimbali zikiwemo za kuwalinda maafisa wanaotenda makosa yakiwemo ya unyanyasaji ndani ya mkoa huo.
Uchunguzi uliofanywa na MorningStarPost umebaini kuwa, kipo kikundi cha baadhi ya maafisa wa Jeshi hilo Mkoani Mbeya, kwa kumtumia askari mmoja anayejulikana kwa jina la Lugome, wanatoa taarifa zenye lengo la kumchafua Kamanda huyo ili aonekane ameshindwa kutimiza majukumu yake.
Imebainika kuwa, mkakati huo ambao ni endelevu, lengo lake ni kuhakikisha Kamanda huyo anahamishwa Mkoani Mbeya ili aje mwingine ambaye atakuwa na maslahi kwa maafisa hao, huku kukiwa na mipango ya kumpigia chapuo mmoja wa maafisa ambaye anadaiwa anatajwa ndiye ana nafasi kubwa ya kushika nafasi hiyo iwapo Kamanda Kuzaga atahamishwa.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, Lugome amekuwa akiwezeshwa kwa namna mbalimbali na maafisa hao ikiwemo kupewa fedha kwa ajili ya kuhakikisha taarifa zinazohitajika zinasambaa kwa jamii na hatimaye Kamanda Kuzaga anahamishwa Mkoani humo na ikibidi apelekwe Makao Makuu kumalizia muda wake.
Tukio ambalo hivi sasa wamepanga kulitumia kwa nguvu kubwa, ni lile la kutekwa, kupigwa na kudhalilishwa kwa msichana anayejulikana kwa jina moja la Farida, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25, ambaye alifanyiwa vitendo hivyo na askari wa kike mwenye cheo cha Sajenti (jina tunalo), ambaye kituo chake cha kazi ni Mbarali.
Inadaiwa, askari huyo amekuwa akimtuhumu msichana huyo kuwa na uhusiano na mume wake ambaye ni mfanyabiashara maarufu mkoani Mbeya, ambapo kwa nyakati tofauti tangu mwishoni mwa mwaka jana, amekuwa akimpiga msichana huyo, kabla ya tukio la hivi karibuni la kumpiga picha za utupu na kuzisambaza mitandoani.
Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, licha ya taarifa kuripotiwa kwenye Kituo cha Polisi Wilayani Mbarali, hakuna hatua zilizochukuliwa kwa muhusika ambaye anaendelea na majukumu yake kwenye ofisi ya upelelezi, huku ikidaiwa yeye (mtuhumiwa) kwa kushirikiana na askari mwenzake wamemchukua msichana huyo na kumuhifadhi, wakimshawishi kuachana na kesi hiyo.
Kutokana na ukimya huo wa Jeshi la Polisi, wanaolenga kumchafua Kamanda Kuzaga wanatumia nafasi hiyo kumuhusisha na mtuhumiwa na kudai ndiye anayemlinda mtuhumiwa, huku wakidai kwamba, mume wa mtuhumiwa naye amekuwa akijigamba kwamba amewaweka mfukoni vigogo wa Jeshi hilo akiwemo RPC.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa, madai hayo hayana ukweli, bali ni mkakati wa kutaka kumuharibia Kamanda Kuzaga, na tayari zipo taarifa kwamba, ufuatiliaji wa wote wanaohusika kujihusisha na mpango umeanza na huenda wakachukuliwa hatua za kinidhamu.
Katika hatua nyingine, inadaiwa ufuatiliaji wa tuhuma zizomkabili askari aliyefanya vitendo vya unyanyasaji na mwenzake anayedaiwa kumficha msichana huyo umeanza na mmoja wa waandishi wa MorningStarPost ameombwa kuwasilisha ushahidi alionao kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo.