NA MWANDISHI WETU

KAMPUNI ya Jandu Construction & Plumbers ya jijini Dar es Salaam imepewa siku 14 kulipa deni la Shilingi Milioni 35,000,000 linalodaiwa na Kampuni ya Kisuse, inayojihusisha na uuzaji na usambazaji wa vipuri vya magari.

Kwa mujibu wa barua yenye Kumbukumbu Na. BIWA20260514/ABT/02 ya Mei 14, 2026, iliyoandikwa na kampuni ya Uwakili ya Black Wings (Black Wings Attonney) na kusainiwa na Yassin Hassan, Jandu wanadaiwa deni hilo tangu mwaka 2019.

Inaelezwa, kati ya Agosti 13, 2019 na Desemba 13, 2019, kampuni ya Kisuse iliipatia kampuni ya Jandu vipuri mbalimbali vya magari, ikiwemo taa za kuashiria, mikanda ya feni, na vifaa vingine vya magari.

“Kwa maombi yenu na kwa makubaliano kwamba malipo yangefanyika kwa wakati unaostahili. Kwa kuamini maelezo na ahadi zenu kwa nia njema, mteja wetu alitimiza wajibu wake kwa kusambaza bidhaa hizo kikamilifu,” ilisema barua hiyo.

Iliendelea “hata hivyo, licha ya kampuni yenu kupokea na kukubali bidhaa hizo, mmeshindwa, mmekataa na/au mmezembea kulipa kiasi kilichobaki, ambacho sasa kinafikia TZS 35,000,000/- (Shilingi Milioni Thelathini na Tano za Kitanzania tu),”

Aidha, barua hiyo iliendelea kudai kuwa, licha ya jitihada zilizofanyika za kufuatilia mara kwa mara deni hilo, Jandu Construction & Plumbers Limited ilitoa ahadi kadhaa za malipo ambazo hazikutekelezwa.

“Zaidi ya hayo, hundi kadhaa zilizotolewa na kampuni yenu kwa ajili ya kulipa deni hilo zilikataliwa benki kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha, jambo linaloonyesha kushindwa kutimiza wajibu wa kifedha pamoja na ukiukwaji wa uaminifu wa kibiashara,” inasomeka barua hiyo ambayo imeelekezwa kwa Mkurugenzi wa Jandu.

Kupitia barua hiyo, imeweka madai kadhaa ambayo yanatakiwa kutekelezwa tangu kupokelewa kwa barua hiyo, ikiwemo malipo ya kiasi chote cha deni cha Shilingi Milioni 35,000,000.

“Malipo yafanywe yote bila punguzo, makato au madai ya kupinga. Pia, ada za kisheria na gharama zote zilizotumika kuanzisha na kuendesha dai hili. Riba itakayoweza kuamriwa na Mahakama. Nafuu nyingine yoyote ambayo Mahakama itaona inafaa na ya haki,” ilisema barua hiyo.

Hata hivyo, mawakili wa mdai kupitia barua hiyo walitoa tahadhari kwamba, “Endapo mtashindwa, mtapuuza na/au mtakataa kutekeleza madai haya ndani ya muda uliowekwa, tuna maelekezo madhubuti ya kuanzisha hatua za kisheria dhidi ya kampuni yenu bila taarifa nyingine zaidi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *