Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imekamilisha ujenzi na ukarabati wa takribani masoko 800 kote nchini, ambapo miundombinu yake imeboreshwa ili kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.
Sambamba na hilo, kipaumbele kimetolewa kwa kundi hilo katika upangaji wa vizimba na maeneo maalum ya wafanyabiashara wadogo ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa TAMISEMI wa Julai 10, 2017 unaoelekeza Halmashauri zote kutenga angalau asilimia 10 ya maeneo ya biashara kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Stella Alex, Aprili 30, 2026, Bungeni jijini Dodoma.
Alisema Serikali inaendelea kutekeleza waraka huo kwa vitendo ili kuhakikisha kundi hilo linapata fursa stahiki katika shughuli za kiuchumi.
Amebainisha kuwa zoezi la utambuzi na usajili wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu linaendelea katika Halmashauri zote nchini, likilenga kuwapa kipaumbele katika upangaji wa vizimba kwenye masoko na maeneo ya wafanyabiashara wadogo.
Aidha, alifafanua kuwa katika baadhi ya maeneo, vizimba hivyo hupangiwa watu wengine pale ambapo walengwa hawajajitokeza, lakini kwa sharti la kuwapisha mara watakapohitaji.
Kadhalika, Halmashauri zimeelekezwa kuimarisha usimamizi ili kuondoa uvamizi wa maeneo hayo na kuweka alama maalum za utambulisho ili yaweze kutambulika kirahisi.
Serikali imeahidi kuendelea kusimamia utekelezaji huo ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wananufaika kikamilifu na fursa za biashara katika masoko hayo.
Katika hatua nyingine, Serikali imeeleza kuwa itatoa orodha kamili ya maeneo na vizimba vilivyotengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu nchini, hatua itakayosaidia kuongeza uwazi na kurahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji wa sera hiyo.